Kampuni kubwa ya uwekezaji ya Japani, SoftBank, imefanya uamuzi wa kutikisa soko la teknolojia duniani, ikiashiria mabadiliko makubwa ya kimkakati kwenye mbio za Akili Mnemba (AI). Katika taarifa yake ya mapato ya robo mwaka iliyotolewa Novemba 11, SoftBank imethibitisha kwamba imeuza hisa zake zote ilizokuwa ikimiliki katika kampuni ya Nvidia—ambayo ndiyo 'mfalme' wa sasa wa utengenezaji wa 'chip' za AI duniani.
Uamuzi huu umetafsiriwa kama hatua ya kijasiri ya bosi wa kampuni hiyo, Masayoshi Son, ili kupata pesa taslimu za kutosha kumwaga kwenye 'dau' lake jipya analoliamini zaidi: OpenAI, kampuni iliyo nyuma ya mafanikio ya ChatGPT.
Mkakati wa Kukusanya Pesa Taslimu
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, SoftBank iliuza hisa zake zote za Nvidia kwa kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 5.83 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 15.15). Uuzaji huu wa hisa milioni 32.1 ulifanyika mwezi Oktoba.
Kama hiyo haitoshi, kampuni hiyo pia iliuza sehemu ya hisa zake katika kampuni ya mawasiliano ya T-Mobile kwa kiasi cha Dola bilioni 9.17 (takriban TZS Trilioni 23.8). Afisa Mkuu wa Fedha wa SoftBank, Yoshimitsu Goto, alieleza kuwa huu ni mkakati wa "kubadilisha mali kuwa pesa taslimu ili waweze kushika fursa mbalimbali za uwekezaji" huku wakilinda afya ya kifedha ya kampuni.
Pesa Yote Yanakwenda Wapi?
Vyanzo vya habari kutoka CNBC vimebainisha kuwa pesa hizi zilizopatikana kutokana na mauzo ya Nvidia ndizo "chanzo kikuu cha fedha" kitakachotumika kufanikisha mpango kabambe wa SoftBank wa kuwekeza Dola bilioni 22.5 (kama TZS Trilioni 58.5) ndani ya OpenAI.
SoftBank inaripotiwa kuhitaji jumla ya Dola bilioni 30.5 (kama TZS Trilioni 79.3) kwa robo hii pekee ili kufadhili miradi yake mbalimbali, ikiwemo ununuzi wa kampuni ya ABB Robotics na uwekezaji huo mkubwa kwa OpenAI.
Soko Latikisika, Hofu ya 'Puto la AI'
Kitendo cha SoftBank 'kutema' hisa zote za Nvidia kiliitikisa kidogo soko la hisa, na kusababisha hisa za Nvidia kushuka kwa asilimia 2. Hali hii imeongeza mafuta kwenye moto wa mjadala unaoendelea mitaa ya Wall Street (soko la hisa la Marekani) kuhusu iwapo soko la AI limefika kiwango cha 'puto la kiuchumi' (AI bubble) linalokaribia kupasuka. Wengi walianza kujiuliza kama Masayoshi Son ameona dalili za hatari ndiyo maana anajiondoa kwenye Nvidia.
Hata hivyo, wataalamu wengi wa uchumi wanaona tofauti. Wanasema huu si kura ya kutokuwa na imani na Nvidia. Badala yake, ni mkakati wa kawaida wa kibiashara wa SoftBank wa kuhamisha fedha kutoka uwekezaji mmoja kwenda mwingine inaouona utakuwa na faida zaidi siku za usoni.
Majuto ya 'Timing' ya Masayoshi Son
Historia ya Masayoshi Son na uwekezaji wake katika Nvidia imejaa 'visa na mikasa'. Anajulikana kwa 'kukosea majira' (mistiming) huko nyuma. Alifanya uamuzi wa kuuza hisa zake nyingi za Nvidia mwaka 2019, kabla tu ya mlipuko mkubwa wa mahitaji ya AI kuanza, na hivyo kukosa faida ya mabilioni ya dola. Baadaye alinunua tena, na sasa anauza tena.
Mchambuzi mmoja alitoa maoni akisema, "Ni vigumu kusema Son amekuwa na mafanikio na 'timing' ya kuuza na kununua hisa za Nvidia," akisisitiza kuwa uamuzi huu mpya unaonekana kuwa ni wa lazima ili kupata pesa za miradi mingine.
Uwekezaji huu mpya utaongeza hisa za SoftBank ndani ya OpenAI kutoka asilimia 4% ya awali hadi kufikia asilimia 11%, ikiwapa sauti kubwa zaidi ndani ya kampuni hiyo inayoongoza mbio za AI. Hata hivyo, imeripotiwa kuwa SoftBank haina mpango wa kuchukua udhibiti kamili wa uongozi wa OpenAI.