Google Yapanga Mapinduzi Dhidi ya Nvidia, Yamshawishi Zuckerberg Kutumia 'Ubongo' Wake Mpya

it | Wed Nov 26 2025


Google Yapanga Mapinduzi Dhidi ya Nvidia, Yamshawishi Zuckerberg Kutumia 'Ubongo' Wake Mpya

Katika kile kinachoonekana kama "vita ya tembo wawili" ambapo nyasi (Nvidia) zinaweza kuanza kuumia, kampuni ya Google imeamua kuvua gwanda na kuingia uwanjani kupambana ana kwa ana na utawala wa Nvidia katika soko la vipuri vya Akili Mnemba (AI Chips). Taarifa za ndani kutoka Silicon Valley zinaeleza kuwa Google ipo katika mazungumzo mazito na kampuni ya Meta (wamiliki wa Facebook, Instagram, na WhatsApp) ili kuwauzia teknolojia yao mpya ya kuchakata data, hatua inayotajwa kama mapinduzi makubwa ya kibiashara.


Google Yataka Tonge la Nvidia


Kwa muda mrefu, Nvidia imekuwa ikitamba kama "Mfalme wa Pori" katika utengenezaji wa 'Graphics Processing Units' (GPUs) ambazo ndizo injini kuu za kuendesha mifumo ya AI duniani. Hata hivyo, Google imeamua kuwa sasa basi. Ripoti kutoka The Information zinaeleza kuwa Google inataka kumpa Mark Zuckerberg na timu yake ya Meta ofa ambayo hawatoweza kuikataa: kutumia chipu zao maalum zinazoitwa 'TPU' (Tensor Processing Units).


Lengo la Google ni wazi na linafahamika: Wanataka kuhakikisha kuwa wanamega angalau asilimia 10 ya mapato yote ya Nvidia. Ikumbukwe kuwa Nvidia imekuwa ikikusanya mabilioni ya dola, na Google anaamini kuwa ana uwezo wa kutoa bidhaa bora kwa bei nafuu zaidi ("Cost-effective alternative").


Silaha Mpya: 'Ironwood' na Mkakati wa "TPU@Premises"


Google haiendi vitani mikono mitupu. Mapema mwezi huu, kampuni hiyo ilitambulisha kizazi chake cha saba cha chipu, kinachojulikana kama TPU ‘Ironwood’ pamoja na CPU mpya iitwayo ‘Axion’. Hizi sio chipu za kawaida; zimetengenezwa mahususi kuhimili mikikimikiki ya kuchakata data nzito za AI kwa kasi ya ajabu.


Lakini "turufu" kubwa ya Google ipo kwenye programu mpya waliyoibuni inayoitwa 'TPU@Premises'. Hii ni programu janja inayolenga kuvunja ngome ya Nvidia. Kwa miaka mingi, Nvidia imewateka wateja wake kupitia mfumo wake wa 'CUDA software', kiasi kwamba ilikuwa vigumu kwa kampuni kuhama. Sasa, 'TPU@Premises' inakuja kama mkombozi, ikiwezesha makampuni makubwa kama Meta kufunga na kutumia chipu za Google kwenye vituo vyao vya data (Data Centers) bila kulazimika kubadilisha mifumo yao yote. Ni kama vile kuwezesha gari la Toyota kutumia spea za Nissan bila shida yoyote.


Mabilioni Mezani na Ushahidi wa Gemini 3


Mazungumzo kati ya Google na Meta si ya "chai ya jioni." Yanahusisha uwekezaji wa mabilioni ya dola. Imeripotiwa kuwa Meta inafikiria kuingiza chipu hizi za TPU kwenye vituo vyao ifikapo mwaka 2027.


Hii inakuja huku kukiwa na ripoti za awali (Agosti mwaka huu) zilizodokeza kuwepo kwa mkataba wa huduma za Wingu (Cloud Computing) kati ya wababe hawa wawili wenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 10 (sawa na takriban Shilingi Trilioni 27 za Kitanzania).


Jeuri ya Google inatoka wapi? Jibu ni Gemini 3. Mfumo huu mpya wa AI wa Google, ambao umepigiwa chapuo kuwa na uwezo mkubwa, ulifunzwa kwa kutumia chipu hizi hizi za TPU. Mafanikio ya Gemini 3 yamekuwa ushahidi tosha kwa wateja watarajiwa kuwa, "Ona, sisi wenyewe tunazitumia na zinafanya kazi kwa ufanisi kuliko za mshindani wetu."


Upanuzi wa Himaya


Google haijaiacha Meta pekee. Mwezi uliopita, ilitanua uhusiano wake na kampuni ya Anthropic (watengenezaji wa Claude AI) kwa kuahidi kuwapatia hadi chipu milioni moja za TPU. Pia, kumekuwa na taarifa kuwa hata OpenAI (waanzilishi wa ChatGPT) walilazimika kuingia mkataba na Google kutokana na msongamano wa watumiaji, jambo linaloonyesha kuwa "miundombinu ya Google ni imara."


Kwa sasa, Google inatanua wavu wake kwa kuwafuatilia watoa huduma wengine wa 'Neo-cloud' kama CoreWeave na Crusoe. Hii ni ishara kuwa soko la teknolojia linatarajia mtikisiko mkubwa. Kwa wafanyabiashara na wapenda teknolojia nchini Tanzania, hii inamaanisha tutarajie kuona ushindani ukishusha gharama za huduma za AI huko tuendako, au kuleta ufanisi mpya kwenye mifumo tunayotumia kila siku.


Kama wahenga wasemavyo, "Fahari wawili wapiganapo, ziumiazo ni nyasi," lakini katika hili, fahari wawili (Google na Nvidia) wakipigana vikumbo, mlaji wa mwisho anaweza kuokota dodo chini ya mwarobaini kwa kupata huduma bora zaidi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.