Anthropic Yachukua Uamuzi Mgumu: Yapanga Kuingia Soko la Hisa Kabla ya OpenAI, Vita ya Mabilioni Yapamba Moto

it | Thu Dec 04 2025


Anthropic Yachukua Uamuzi Mgumu: Yapanga Kuingia Soko la Hisa Kabla ya OpenAI, Vita ya Mabilioni Yapamba Moto

Katika kile kinachoonekana kama "mbio za sakafuni" kuelekea kwenye kilele cha utajiri wa kidijitali, kampuni ya Akili Mnemba (AI) ya Anthropic, inayotamba na roboti yake ya Claude, imeripotiwa kuanza maandalizi ya siri ya kuuza hisa zake kwa umma (Initial Public Offering - IPO). Hatua hii inatazamwa kama mkakati wa kijanja wa kuuwahi mpinzani wake mkuu, OpenAI (wamiliki wa ChatGPT), na kuteka soko la mitaji duniani.


Ripoti za kiuchumi kutoka gazeti la Financial Times zinadokeza kuwa Anthropic imeungana na kampuni nguli ya sheria ya Wilson Sonsini ili kusimamia mchakato huo ambao unatajwa kuwa unaweza kuwa IPO kubwa zaidi katika historia ya teknolojia.


Vita ya "Nani atawahi Sokoni?"


Chanzo cha habari kimeliambia gazeti hilo kuwa Anthropic inataka kufanya jambo ambalo OpenAI bado inalisuasua. Wakati OpenAI ikitajwa kuwa na mpango wa kuingia soko la hisa mwaka 2027 huku ikisisitiza kujenga miundombinu kwanza, wawekezaji wa Anthropic wanashinikiza kampuni hiyo iingie sokoni mapema, pengine mwaka 2026, ili kupata "First-Mover Advantage" (Faida ya Kuwa wa Kwanza).


Wawekezaji hao wanaamini kuwa yule atakayewahi kuweka hisa zake mezani ndiye atakayekusanya fedha nyingi zaidi kutoka kwa wenye nazo, na hivyo kupata mtaji wa kutosha wa kumpiku mwingine kwenye utafiti na maendeleo.


Wilson Sonsini, kampuni ya sheria iliyopewa jukumu hili, si ya mchezo. Hawa ndio waliowahi kusimamia uuzwaji wa hisa za makampuni makubwa kama Google, LinkedIn, na Lyft. Hivyo, kuwepo kwao ni ishara tosha kuwa Anthropic haitanii.


Thamani ya Kutisha: Trilioni 945 Mezani


Mwezi uliopita, Anthropic iligonga vichwa vya habari kwa kupokea uwekezaji wa Dola bilioni 15 kutoka kwa Microsoft na NVIDIA. Uwekezaji huo uliifanya kampuni hiyo kuthaminiwa kuwa na thamani ya Dola bilioni 350 (sawa na takriban Shilingi Trilioni 945 za Kitanzania).


Kwa upande wa pili, OpenAI inashikilia rekodi ya kuwa kampuni binafsi (Private Company) yenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, ikikadiriwa kufika Dola bilioni 500 (Takriban Shilingi Trilioni 1,350). Vita hii ya namba inaonyesha ni kwa kiasi gani wawekezaji wana imani na teknolojia hii mpya.


Maandalizi ya Ndani: Kumsajili "Mchawi" wa Airbnb


Kama ishara ya kuwa wako serious, mwaka jana Anthropic ilimsajili Krishna Rao kuwa Afisa Mkuu wa Fedha (CFO). Rao anajulikana soko la hisa kwa kazi yake nzuri ya kusimamia kuingia sokoni kwa kampuni ya Airbnb. Ujio wake unatafsiriwa kama "kupanga safu" tayari kwa mechi kubwa ya soko la hisa.


Kigugumizi cha Faida


Hata hivyo, wachumi wanatoa angalizo. Licha ya thamani kubwa wanayopewa, ukweli mchungu ni kwamba kampuni zote mbili—Anthropic na OpenAI—bado zinaingiza hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka. Gharama za kuendesha mitambo ya AI (Servers na Umeme) ni kubwa mno kuliko mapato wanayopata sasa.


Hali hii ya kutotengeneza faida (Profitability) inaweza kuwa kikwazo kikubwa wakati wa kuuza hisa, kwani wawekezaji wa soko la hisa hupenda kuona faida, tofauti na wawekezaji wa mitaji hatarishi (Venture Capitalists) ambao huangalia ukuaji.


Msemaji wa Anthropic amejaribu kupoza moto kwa kusema: "Kampuni yenye ukubwa na mapato kama yetu kuendeshwa kama kampuni ya umma ni jambo la kawaida... lakini kwa sasa hatuna tangazo rasmi la lini tutaingia sokoni."


Kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania wanaofuatilia masoko ya kimataifa, hii ni "Space Watch" ya kipekee. Kuingia kwa Anthropic soko la hisa kutafungua ukurasa mpya wa jinsi teknolojia ya AI inavyorithisha au kufilisi wawekezaji.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.