Kutoka Visiwani Hadi Bara: Wasomi wa SUZA 'Wafukua' Hazina ya Karne Ngorongoro

it | Mon Nov 24 2025


Kutoka Visiwani Hadi Bara: Wasomi wa SUZA 'Wafukua' Hazina ya Karne Ngorongoro

Katika hatua ya kuimarisha elimu kwa vitendo na kuenzi historia ya kale ya dunia, wasomi na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wamefanya ziara ya kihistoria katika hifadhi ya pekee ya Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark, iliyopo wilayani Karatu, mkoani Arusha. Safari hii ya kielimu imetajwa kuwa ni mapinduzi makubwa katika ufundishaji wa fani ya akiolojia nchini, ikilenga kuwatoa wanafunzi katika nadharia za darasani na kuwapeleka katika uhalisia wa kisayansi.


Eneo hili la Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai si kivutio cha kawaida; linabeba sifa ya kipekee kama Jiopaki pekee iliyopo Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye volkano hai ya mlima Oldoinyo Lengai (Mlima wa Mungu). Barani Afrika nzima, hii ni ya pili kwa hadhi hiyo, ikitanguliwa na Jiopaki ya M'Goun iliyopo nchini Morocco, jambo linaloifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha tafiti za jiolojia duniani.


Darasa la Dunia Ndani ya Bonde la Ufa Akizungumza kwa hisia baada ya kuhitimisha mafunzo hayo ya vitendo mwishoni mwa wiki, Mhadhiri wa SUZA, Dk. Abdallah Mkumbukwa, alibainisha kuwa makumbusho hayo yamegeuka kuwa 'maabara hai' kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Alisema kuwa fursa ya kujifunza katika eneo hilo ni adimu na inawajengea wanafunzi umahiri usiotiliwa shaka katika masuala ya miamba na chimbuko la binadamu.


"Tumetoka Visiwani kuja hapa Bara kujifunza kwa vitendo. Hili ni darasa kubwa sana kwa wanafunzi wetu wa SUZA. Tumeshuhudia muunganiko wa ajabu kati ya nadharia tulizowafundisha darasani na uhalisia wa mazingira. Hapa ni kisima cha elimu ya miamba, jiolojia na utamaduni," alisema Dk. Mkumbukwa.


Aliongeza kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kuchunguza miamba yenye umri wa zaidi ya miaka milioni tatu, jambo ambalo linawapa picha halisi ya mabadiliko ya dunia na mfumo wa Bonde la Ufa (Rift Valley) unavyoathiri maumbile ya nchi.


Muingiliano wa Sayansi na Utamaduni Mbali na sayansi ya miamba, ziara hiyo iliwapa wasomi hao nafasi ya kuchota hekima za asili kutoka kwa jamii zinazozunguka eneo hilo. Ngorongoro-Lengai ni nyumbani kwa makabila yenye tamaduni za kipekee ambazo hazijachafuliwa na utandawazi, wakiwemo Wahadzabe (wawindaji na waokota matunda), Wadatoga (wafua vyuma), Wairaqw na Wamasai wafugaji. Mchanganyiko huu wa akiolojia na anthropolojia unatoa wigo mpana wa kuelewa maisha ya kale na sasa.


Kwa upande wake, Msimamizi wa Makumbusho ya Jiopaki hiyo, Afisa Uhifadhi Mkuu Dk. Agness Gidna, ameleza kufurahishwa kwake na mwitikio wa taasisi za elimu. Amesema tangu kufunguliwa rasmi kwa makumbusho hiyo mwezi Oktoba mwaka huu, imekuwa sumaku ya kuvutia wageni, si tu kwa ajili ya kutalii bali kuchimba maarifa.


"Hapa tunatoa kitu cha ziada. Wageni wanaokuja, wakiwemo hawa wa SUZA, wanaondoka na uelewa mpana wa historia ya sayansi, mazingira na urithi wetu wa utamaduni. Ni faraja kuona elimu ya akiolojia inaanza kupewa uzito unaostahili hapa nchini kupitia makumbusho yetu," alisisitiza Dk. Gidna.


Ziara hii ya SUZA ni kielelezo cha ushirikiano wa kitaaluma unaopaswa kuigwa, ukisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za ndani kukuza taaluma na utalii wa kielimu nchini Tanzania.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.