ChatGPT Yagonga Ukuta Ujerumani: Mahakama Yaamuru OpenAI Kutoa Fidia Kwenye Kesi ya Wizi wa Mashairi

it | Thu Nov 13 2025


ChatGPT Yagonga Ukuta Ujerumani: Mahakama Yaamuru OpenAI Kutoa Fidia Kwenye Kesi ya Wizi wa Mashairi

Hatimaye 'mnyama' wa Akili Mnemba (AI), kampuni ya OpenAI, amekutana na kisiki cha mpingo nchini Ujerumani. Katika pigo kubwa ambalo linaweza kubadilisha kabisa jinsi kampuni za AI zinavyofanya kazi duniani kote, Mahakama ya Wilaya ya Munich imetoa hukumu kwamba ChatGPT ilivunja sheria za hakimiliki kwa kutoa upya mashairi ya nyimbo bila ruhusa.


Hukumu hii ya kihistoria ni ya kwanza kabisa kumkuta OpenAI na hatia ya ukiukwaji wa hakimiliki na kuamriwa kulipa fidia, ikiweka mwelekeo mpya wa kisheria utakaotikisa tasnia nzima ya AI.


Kesi hii ilifunguliwa na Taasisi ya Haki za Muziki ya Ujerumani (GEMA), ambayo ni kama 'COSOTA' ya huko Ujerumani, ikiwakilisha zaidi ya watunzi, waandishi wa nyimbo, na wachapishaji wa muziki 80,000. GEMA walilalamika kuwa ChatGPT ilikuwa ikitumia na kutoa upya mashairi ya nyimbo maarufu za Kijerumani, ikiwemo nyimbo tisa za mwanamuziki nguli nchini humo, Herbert Grönemeyer (kama vile ‘Maenner’ na ‘Bochum’), bila idhini wala malipo.


Utetezi wa OpenAI Wapigwa Chini


Wakati wa kesi, OpenAI walijaribu kutumia utetezi wao wa kawaida. Walidai kuwa ChatGPT 'haihifadhi' wala 'kunakili' data fulani kama vile mashairi. Badala yake, walidai kuwa mfumo wao 'unajifunza ruwaza' (patterns) kutoka kwenye lundo kubwa la data walilolitumia kuifundisha. Zaidi ya hayo, walijaribu kuhamishia lawama kwa mtumiaji, wakisema kuwa kama AI ilitoa mashairi hayo, ni kwa sababu mtumiaji aliiagiza (kwa kutumia 'prompt') kufanya hivyo, na hivyo lawama zinapaswa kumwangukia mtumiaji.


Hata hivyo, Mahakama ya Munich ilikataa katakata utetezi huu. Katika uamuzi wake, Jaji Elke Schwager alitoa msimamo mkali:


  1. Alisema kitendo chenyewe cha mfumo wa AI "kukariri" (memorization) mashairi hayo wakati wa mafunzo yake ni ukiukwaji wa hakimiliki.
  2. Pili, kitendo cha 'chatbot' hiyo kutoa upya (reproduce) mashairi hayo kwa mtumiaji ni uvunjaji mwingine wa haki za mtunzi.


Ingawa kiwango kamili cha fidia (damages) hakijawekwa wazi, uamuzi wenyewe wa kutaka OpenAI walipe ni ushindi mkubwa kwa wasanii.


GEMA Yashangilia, OpenAI Yakasirika


Baada ya ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa GEMA, Tobias Holtzmüller, alitoa kauli kali: "Intaneti siyo duka la kujihudumia (self-service store), na ubunifu wa binadamu si kiolezo cha bure ambacho mtu yeyote anaweza kuchukua na kutumia. Hukumu hii inaweka rekodi muhimu kwamba hata kampuni za AI lazima zifuate sheria za hakimiliki."


Kwa upande wao, OpenAI walionyesha kutokubaliana na uamuzi huo. Katika taarifa yao, walidai kuwa hukumu hiyo "inawahusu idadi ndogo sana ya mashairi" na kwamba "haitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mamilioni ya watumiaji na wafanyabiashara nchini Ujerumani." Walisema hawakubaliani na uamuzi huo na wanatafakari hatua zaidi za kisheria watakazochukua.


Hukumu hii ni moja ya maamuzi makuu ya kwanza duniani kushughulikia moja kwa moja swali la iwapo ni halali kwa AI kutumia kazi zenye hakimiliki (kama muziki, vitabu, na sanaa) kama data ya mafunzo. Inatarajiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa sheria na udhibiti wa AI barani Ulaya na duniani kote.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.