Vita kati ya vyombo vya habari vya zamani (Traditional Media) na kampuni mpya za teknolojia (AI Startups) imefikia pabaya. Gazeti linaheshimika zaidi duniani, The New York Times (NYT), limeamua kuburuza mahakamani kampuni ya Perplexity AI, likiituhumu kwa "wizi wa mchana kweupe" wa maudhui yake.
NYT imefungua mashtaka hayo katika Mahakama ya Kusini ya New York, ikidai kuwa Perplexity imekuwa ikinakili na kusambaza habari, video, na makala zao bila ruhusa ili kujenga biashara yake. Hii ni kesi ya kihistoria inayoashiria kuwa vyombo vya habari vimechoka kuona kazi zao zikitumiwa na AI kutengeneza pesa bila wao kunufaika.
Tuhuma Nzito: "Mnakunywa Jasho Letu Bure"
Katika hati ya mashtaka, NYT inadai kuwa Perplexity inatumia roboti (crawlers) kupenya kwenye tovuti yao na kuchota habari, hata zile ambazo wasomaji wanalipia (Paywall).
NYT imetoa madai makuu mawili:
- Wizi wa Maudhui: Perplexity inatoa majibu ambayo yanafanana kabisa na makala za NYT, jambo linalofanya wasomaji wasiende kusoma kwenye gazeti hilo.
- Uchafuzi wa Jina: Wakati mwingine, Perplexity inatunga uongo (hallucinations) na kudai kuwa habari hiyo imetoka NYT, jambo linaloharibu sifa ya gazeti hilo.
Msemaji wa NYT, Graham James, amesema: "Tunaunga mkono maendeleo ya AI yenye maadili, lakini tunapinga vikali matumizi ya jasho letu bila idhini. Tutawawajibisha wote wasioheshimu thamani ya uandishi wa habari."
Perplexity Yajitetea: "Huu ni Wivu wa Maendeleo"
Kampuni ya Perplexity imekanusha tuhuma hizo ikidai kuwa NYT inapiga kelele zilezile zilizopigwa na magazeti wakati Redio, TV, na Intaneti vilipozaliwa.
Jesse Dwyer, mkuu wa mawasiliano wa Perplexity, amedai kuwa wao hawafanyi "Scraping" kwa ajili ya kufundisha mitambo yao, bali wanafanya "Indexing" (kuorodhesha) kama inavyofanya Google ili kutoa majibu na vyanzo.
Msururu wa Kesi: Perplexity Iko Matatani
Inaonekana Perplexity imewachokoza wengi. NYT si pekee inayolia nao. Kampuni hiyo inakabiliwa na mvua ya kesi kutoka pande zote za dunia:
- Chicago Tribune (Marekani)
- RTI na Medusa Film (Italia) - Kwa kuiba filamu na vipindi vya TV.
- Britannica (Kamusi elezo)
- Magazeti ya Japani (Yomiuri, Nikkei, Asahi)
- News Corp (Wamiliki wa Wall Street Journal)
Tatizo kubwa ni kwamba wakati Google na OpenAI wameanza kuingia mikataba na kulipa vyombo vya habari, Perplexity ilichelewa kuja na mfumo wa kugawa mapato (Revenue Sharing), na hivyo kuonekana kama "kupe" anayefyonza damu bila kutoa chochote.
Vita ya Wakubwa
Hii si vita ndogo. NYT tayari ina kesi nyingine inayoendelea dhidi ya OpenAI na Microsoft kwa tuhuma hizohizo. Hata hivyo, inashirikiana vyema na Amazon, ikiwa na maana kuwa tatizo si teknolojia, bali ni "Hela."
Kwa Tanzania na Afrika Mashariki, kesi hii ni funzo kuwa sheria za hakimiliki (Copyright) katika zama za AI zinazidi kukazwa. Waundaji wa maudhui wanapaswa kulindwa dhidi ya mitambo inayoweza kuchukua kazi zao na kuziuza upya bila wao kupata senti.