Fikiria unapokuwa bafuni na kuona nywele zimekusanyika kwenye njia ya maji. Unachofanya ni kuzikusanya na kuzisokota kwa viganja vyako hadi kuwa tufe dogo ambalo ni rahisi kuliondoa. Sasa, wanasayansi kutoka Marekani wametumia wazo hili rahisi la kila siku kubuni teknolojia ya kimapinduzi inayoweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walio katika hatari ya kupata shambulio la moyo na kiharusi (strok).
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, wakiongozwa na Profesa Ruike Renee Zhao na Profesa Jeremy Heit, wamegundua mbinu ya kuondoa mabonge ya damu (thrombus) yanayoziba mishipa kwa kuyasokota na kuyapunguza ukubwa, kama vile unavyofanya kwa nywele. Ugunduzi huu wa ajabu ulichapishwa hivi karibuni katika jarida maarufu la kimataifa la sayansi, 'Nature'.
Mabonge haya ya damu huundwa na protini nyembamba kama nyuzi ziitwazo ‘fibrin’ ambazo hunasa chembe nyekundu za damu na kutengeneza donge nene linalonata. Donge hili likiziba mshipa unaopeleka oksijeni kwenye ubongo, husababisha kiharusi, na likiziba mshipa wa moyo, husababisha shambulio la moyo. Katika hali hizi, madaktari hushindana na muda ili kuondoa donge hilo haraka iwezekanavyo ili kuokoa seli za ubongo au misuli ya moyo.
Hata hivyo, mbinu za sasa za kuondoa mabonge haya zina changamoto. Madaktari hutumia vifaa vinavyofyonza donge kama ‘vacuum cleaner’ au wavu maalum wa metali unaoitwa ‘stent’ kulivuta. Cha kusikitisha, uwezekano wa kufanikiwa katika jaribio la kwanza ni asilimia 50 tu. Mbaya zaidi, wakati mwingine donge huvunjika na vipande vidogo huenda kukwama kwenye mishipa myembamba zaidi, na kufanya hali kuwa mbaya zaidi.
Teknolojia mpya ya Stanford inatumia kifaa kidogo sana kinachozunguka ('milli-spinner') kinachoingizwa kwenye mshipa wa damu. Kifaa hiki kinapozunguka, kinatumia nguvu ya mkandamizo na msuguano (compression and shear force) kulikandamiza donge la damu. Kama vile nywele zinavyosokotana, nyuzi za fibrin hujikusanya pamoja na kuwa tufe dogo na gumu, huku zikiachia chembe nyekundu za damu ziendelee na safari yake kwenye mzunguko wa damu.
Profesa Zhao alieleza, "Katika majaribio yetu kwenye mishipa ya bandia na kwenye nguruwe, tuliweza kupunguza ukubwa wa donge la damu hadi kufikia asilimia 5 ya ukubwa wake wa awali." Hii inafanya iwe rahisi sana kuliondoa bila hatari ya kulivunja. Matokeo yalikuwa ya kuvutia: teknolojia hii ilifanikiwa kuondoa asilimia 90 ya hata yale mabonge magumu zaidi katika jaribio la kwanza.
Cha kufurahisha ni kwamba, wazo hili lilizaliwa kwa bahati wakati Profesa Zhao alipokuwa akitengeneza roboti ndogo sana za kutembea ndani ya mishipa ya damu. Aligundua kuwa kifaa cha mzunguko cha roboti hiyo kilitengeneza nguvu ya uvutaji iliyoweza kukusanya vitu. Kutoka hapo, wazo la kutibu mabonge ya damu likazaliwa.
Watafiti hawa sasa wameanzisha kampuni (startup) ili kuifanyia biashara teknolojia hii na wanapanga kuanza majaribio ya kliniki kwa binadamu hivi karibuni. Zaidi ya hapo, wanaangalia uwezekano wa kutumia mbinu hii kuondoa vipande vya mawe kwenye figo, kuonyesha jinsi wazo rahisi la kila siku linavyoweza kuleta mapinduzi makubwa katika dunia ya tiba.