Katika nchi yetu ya Tanzania, ambapo kilimo ni uti wa mgongo na wavuvi hutegemea bahari kuchuma riziki, kubadilika kwa hali ya hewa bila taarifa sahihi kumekuwa changamoto kubwa. Mara nyingi tumesikia wakulima wakilalamika mvua kunyesha wakati hawakutarajia, au kukauka wakati mazao yanahitaji maji. Lakini sasa, kampuni ya Google kupitia kitengo chake cha Google DeepMind, imekuja na suluhisho la kiteknolojia linaloweza kuwa 'mkombozi' kwa sekta hizi nyeti.
Hapo jana, Google DeepMind ilizindua rasmi mtambo mpya wa Akili Mnemba (AI) uitwao 'WeatherNext 2'. Huu si mtambo wa kawaida wa kutabiri kama mvua itanyesha au la; ni mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kuchambua hali ya hewa kwa kasi ya ajabu na kwa usahihi wa hali ya juu ambao haujawahi kushuhudiwa.
Kutabiri Saa kwa Saa, Siyo Asubuhi na Jioni Tu
Tofauti na mifumo ya zamani iliyozoeleka kutoa taarifa za jumla (kwa mfano, "kutakuwa na mvua nyakati za mchana"), WeatherNext 2 ina uwezo wa kutoa utabiri wa saa kwa saa. Hii ina maana mkulima wa Morogoro anaweza kuambiwa, "Mvua itaanza kunyesha saa nne kamili asubuhi na kukata saa tano." Uwezo huu wa saa kwa saa (hourly forecast) ni mapinduzi makubwa yanayosaidia watu kupanga kazi zao kwa ufanisi zaidi, iwe ni kupanda, kuvuna, au kusafirisha mizigo.
Kasi ya 'Jet' na Usahihi wa Vimbunga
Kitu kingine kinachofanya mfumo huu kuwa wa kipekee ni kasi yake. Google wanasema WeatherNext 2 inafanya kazi mara 8 zaidi ya mifumo iliyopita. Hii inatokana na kubadili jinsi inavyochakata data; badala ya kufanya mahesabu yanayojirudia kama kuchora video, inafanya hesabu moja kubwa na kutoa jibu papo hapo.
Kwa wakazi wa maeneo ya Pwani kama Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar, ambao mara kwa mara hukumbwa na hofu ya vimbunga (kama vile Kimbunga Hidaya kilichotutishia hivi karibuni), teknolojia hii ina habari njema. AI hii imeonyesha uwezo wa kutabiri njia ya kimbunga au dhoruba kali siku tatu (3) kabla ya tukio, kwa usahihi mkubwa. Hii ni hatua moja mbele ukilinganisha na mifumo ya zamani iliyokuwa ikitoa uhakika wa siku mbili tu. Siku hiyo moja ya ziada inaweza kuokoa maisha na mali nyingi kwa kutoa nafasi ya kujiandaa mapema.
Biashara na Nishati
Faida za WeatherNext 2 haziishii kwa wakulima tu. Sekta ya nishati inatarajia kunufaika sana. Kwa makampuni yanayozalisha umeme wa upepo au jua, kujua hali ya hewa kwa kila saa kunawasaidia kukadiria kiasi gani cha umeme kitazalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa. Pia, makampuni ya bima na usafirishaji wa mizigo yataweza kupunguza hasara zinazotokana na majanga ya asili kwa kupata taarifa mapema.
Bado Kuna Changamoto
Hata hivyo, Google wamekiri kuwa "mganga" huyu wa kidijitali bado hajamaliza kila tatizo. Mfumo huu bado una kigugumizi linapokuja suala la kutabiri matukio ya ghafla sana na yaliyopitiliza, kama vile mafuriko makubwa ya ghafla au mvua za mawe. Hii inatokana na ukweli kwamba data za matukio haya adimu bado hazitoshelezi kuifundisha AI kikamilifu.
Hii inaashiria kuwa vita ya kutawala anga la utabiri wa hali ya hewa imepamba moto. Google sasa inachuana vikali na vigogo wengine kama Nvidia, Microsoft, Huawei, na Kituo cha Utabiri cha Ulaya (ECMWF) kuona nani atakuwa mfalme wa kutabiri kesho yetu. Kwa Tanzania, kadiri teknolojia hizi zinavyozidi kuwa bora, ndivyo tunavyozidi kupata nyenzo za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.