Dunia ya teknolojia imepata mtikisiko mpya na wa kusisimua baada ya kampuni ya Google DeepMind kutangaza hatua kubwa kuelekea ndoto ya muda mrefu ya wanasayansi: kuunda mashine yenye akili inayolingana na ya binadamu (AGI). Tarehe 13 Novemba, kampuni hiyo ilizindua 'SIMA 2', toleo jipya la mfumo wa Akili Mnemba (AI) ambalo lina uwezo wa kipekee wa kuishi, kufikiri, na kutenda ndani ya ulimwengu wa kidijitali (3D virtual environments) kama binadamu.
Kama unakumbuka michezo ya video (video games) ambapo unamlazimisha mchezaji kufanya unachotaka, sasa vuta picha mchezaji huyo akiwa na akili yake mwenyewe, anayejua nini cha kufanya bila kuongozwa kila hatua. Hiyo ndiyo SIMA 2.
Tofauti na toleo la kwanza lililotoka mwezi Machi ambalo lilikuwa linafuata maagizo tu kama roboti la kawaida, SIMA 2 imeunganishwa na 'injini' ya akili ya Gemini ya Google. Hii imeipa uwezo wa "kufikiri na kuchambua mambo." Kwa mfano, ukimwambia "Nenda kwenye nyumba yenye rangi ya nyanya iliyoiva," SIMA 2 itafikiri kwanza: "Nyanya iliyoiva ina rangi nyekundu, kwa hiyo natafuta nyumba nyekundu," na kisha itaanza safari. Hii ni hatua kubwa ya kimantiki ambayo mashine nyingi hazina.
Kitu cha kushangaza zaidi ni jinsi SIMA 2 inavyofanya kazi na mfumo mwingine uitwao 'Genie 3'. Mkurugenzi wa DeepMind, Demis Hassabis, anaelezea hili kama "AI moja kuishi ndani ya akili ya AI nyingine."
Kwa lugha nyepesi, ni hivi: Kabla AI haijafanya maamuzi katika dunia halisi (ambayo inaweza kuwa na hatari), inajaribu maamuzi hayo ndani ya ulimwengu wa kufikirika (simulation) uliotengenezwa na Genie 3. Hii inaruhusu AI kujifunza makosa yake na kujirekebisha kabla ya kutenda kosa hilo kweli.
Uwezo wa kujifunza wa SIMA 2 ni wa kutisha. Inaweza kuchukua ujuzi ilioupata kwenye mchezo mmoja (kama kuchimba madini) na kuutumia kwenye mchezo mwingine tofauti kabisa (kama kuvuna mazao), kitu kinachoitwa 'transfer learning'. Awali inajifunza kwa kuangalia binadamu, lakini baadaye inaendelea kujifunza yenyewe bila msaada, ikijaribu mbinu mpya na kuboresha utendaji wake kwa njia ya 'kujaribu na kukosea' (trial and error).
Hatua hii inakuja siku moja tu baada ya kampuni ya WorldLabs ya Profesa Fei-Fei Li kuzindua 'Marble', mfumo mwingine wa kuunda ulimwengu wa kidijitali. Lakini Google wanaonekana kuwa na turufu mkononi kwa kuwa na vyote viwili: AI inayoweza kuunda dunia (Genie 3) na AI inayoweza kuishi na kutenda ndani ya dunia hiyo (SIMA 2).
Hii siyo tu kuhusu michezo ya kompyuta. Wataalamu wanasema teknolojia hizi ndizo msingi wa kuunda roboti za baadaye ambazo zitaweza kufanya kazi katika mazingira yetu ya nyumbani na viwandani, zikiwa na uwezo wa kuelewa maagizo magumu na kutumia vifaa kwa usahihi kama binadamu. Google DeepMind wameonyesha kuwa safari ya kuelekea AGI imepiga hatua kubwa sana.