Habari njema kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, watafiti, na wafanyakazi wote wanaohangaika na kuandaa ripoti nzito. Kampuni ya Google imeongeza nguvu mpya kwenye kifaa chake maarufu cha Akili Mnemba (AI) kiitwacho 'NotebookLM', na kukifanya kuwa msaidizi wa utafiti asiyeshindwa. Katika sasisho jipya lililotangazwa Novemba 13, Google wameongeza kipengele cha 'Deep Research' (Utafutaji wa Kina) ambacho kinaweza kubadilisha kabisa jinsi tunavyokusanya taarifa mtandaoni.
Fikiria una jukumu la kuandika ripoti kuhusu "Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwenye Kilimo cha Korosho Mtwara." Zamani, ingekubidi utafute mwenyewe tovuti moja baada ya nyingine, usome makala ndefu, na kuungaunga taarifa. Sasa, 'NotebookLM' inafanya kazi hiyo kama una msaidizi binafsi wa utafiti (Research Assistant).
Unapoiuliza swali, AI hii haikupi majibu mepesi tu. Inatengeneza mpango kazi, inazunguka kwenye tovuti mbalimbali, inasoma machapisho na ripoti za kitaalamu, kisha inakuandikia ripoti iliyokamilika ikiwa na vyanzo vya uhakika (citations). Google wanasema ni kama "kuajiri mtafiti maalum wa kukufanyia kazi."
Mtumiaji ana uhuru wa kuchagua kati ya njia mbili:
- Fast Research (Utafutaji wa Haraka): Hii inakupa muhtasari wa chapchap kwa ajili ya kupata picha ya haraka ya jambo.
- Deep Research (Utafutaji wa Kina): Hii inachimba ndani zaidi, ikitafuta vyanzo vyenye kuaminika na kutoa uchambuzi wa kina, kitu ambacho ni muhimu sana kwa kazi za kitaaluma.
Mbali na uwezo huo wa kutafuta, Google wamerahisisha maisha kwa kuongeza aina ya mafaili yanayokubalika. Sasa unaweza kupakia faili la Google Sheets (kama Excel) na AI itakusaidia kuchambua takwimu na kutoa muhtasari. Pia, hauna haja tena ya kupakua na kupakia tena mafaili ya PDF mazito; unaweza tu kuweka kiunganishi (link) cha faili lililo kwenye Google Drive yako au hata faili la Microsoft Word, na 'NotebookLM' italisoma na kulichambua papo hapo.
Hii ni hatua kubwa kwa Google katika kuhakikisha kifaa hiki, ambacho kilizinduliwa mwishoni mwa 2023 na kupata umaarufu mkubwa, kinazidi kuwa msaada kwa watumiaji. Ikumbukwe kuwa mwezi Mei mwaka huu, walizindua pia programu ya simu (App) ya kifaa hiki, na kufanya iwe rahisi kwa Watanzania wengi wanaotumia simu janja kufanya tafiti zao popote walipo. Sasisho hili jipya linatarajiwa kuwafikia watumiaji wote ndani ya wiki moja ijayo.