Google Yaliamsha Dude: Yazindua 'Gemini 3' Kumalizana na GPT-5, Yatawala Kwenye 'Coding' na Utafutaji!

it | Wed Nov 19 2025


Google Yaliamsha Dude: Yazindua 'Gemini 3' Kumalizana na GPT-5, Yatawala Kwenye 'Coding' na Utafutaji!

Vita ya wababe wa teknolojia duniani imezidi kupamba moto na sasa tunaweza kusema rasmi kuwa "glavu zimevuliwa." Wiki moja tu baada ya kampuni ya OpenAI kutikisa soko kwa kuzindua toleo lao la 'GPT-5.1', kampuni ya Google imejibu mapigo kwa kishindo kizito kisichotarajiwa. Wamezindua rasmi mfumo wao mpya na wenye nguvu zaidi wa Akili Mnemba (AI) uitwao 'Gemini 3'.


Hili si toleo la kawaida la kuboresha programu; Google wanasema huu ni mfumo mpya kabisa unaoleta mapinduzi katika jinsi mashine zinavyofikiri, kuona, na kusaidia wanadamu. Mkurugenzi Mtendaji wa Google, Sundar Pichai, amesema wazi: "Ndani ya miaka miwili tu, tumetoka kwenye AI inayosoma maandishi hadi kufikia AI inayoelewa mazingira yanayoizunguka kama binadamu."


Gemini 3 ni Nini Hasa na Ina Jipya Gani?


Mfumo huu mpya umekuja na maboresho makubwa matatu ambayo yanaweka kiwango kipya kwenye soko:


  1. Akili ya 'Deep Think' (Kufikiri kwa Kina): Google wameanzisha mfumo mpya unaoitwa 'Gemini 3 Deep Think'. Tofauti na AI za zamani zinazokimbilia kujibu haraka (na wakati mwingine kukosea), mfumo huu unachukua muda "kutafakari" na kupanga hoja zake kabla ya kujibu, hasa kwenye maswali magumu ya hisabati na sayansi. Katika majaribio ya 'Inference' (kufanya maamuzi ya kimantiki), toleo hili limeweka rekodi ya dunia kwa kupata alama 45.1% kwenye mtihani mgumu wa ARC-AGI-2, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na mashine yoyote. Hii ni habari njema kwa watafiti na wanafunzi wa vyuo vikuu hapa Tanzania wanaohitaji uchambuzi wa kina.
  2. Mapinduzi ya 'Coding' na 'Antigravity': Kwa watengenezaji wa programu (developers) wa Silicon Dar na kwingineko, Google imezindua jukwaa jipya liitwalo 'Google Antigravity'. Hii ni sehemu maalum (IDE) inayotumia Gemini 3 kusaidia kuandika kodi za kompyuta. Mfumo huu una uwezo wa 'Vibe Coding'—yaani unaweza kuelewa unataka kutengeneza nini hata kama hujui kuelezea kitaalamu sana. Kwenye majaribio ya kutumia 'Terminal' na kuandika programu, Gemini 3 imeipiga bao toleo la zamani la 2.5 Pro kwa mbali sana (76.2% dhidi ya asilimia za chini).
  3. Ushindi Dhidi ya GPT-5: Kwenye ulimwengu wa AI, namba hazidanganyi. Kwenye mtihani unaoitwa "Humanity’s Last Exam (HLE)"—ambao hupima uelewa wa juu wa kibinadamu—Gemini 3 imepata alama 37.5%, huku mshindani wake mkubwa 'GPT-5 Pro' akiambulia 31.64%. Hii inaashiria kuwa Google wamefanikiwa kutengeneza "ubongo" wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuelewa mambo magumu.


Meneja wa Biashara Asiyechoka


Kitu kingine cha kushangaza ni uwezo wa Gemini 3 kufanya kazi kama "Wakala" (Agent). Katika jaribio la kipekee lililoitwa 'Vending-Bench 2', AI hii ilipewa jukumu la kusimamia biashara ya mashine za kuuza bidhaa (vending machines) kwa muda wa mwaka mzima (kwenye mfumo wa kuigiza). Matokeo yake? Ilifanikiwa kufanya maamuzi sahihi, kutumia vifaa vya kazi, na kutengeneza faida kubwa bila kupoteza mwelekeo hata mara moja. Hii inaonyesha uwezo wa AI kusimamia miradi ya muda mrefu bila kuchoka au kusahau.


Inapatikana Wapi?


Habari njema ni kwamba Google haijaiweka teknolojia hii kabatini. Imeunganishwa moja kwa moja kwenye Google Search (utafutaji wa Google), programu ya Gemini App, na kwa watengenezaji programu kupitia Vertex AI. Hii ina maana watumiaji wa kawaida wataanza kuona majibu bora zaidi na ya haraka wanapotafuta taarifa mtandaoni.


Hata hivyo, huduma ya 'Deep Think' itaanza kupatikana kwa watumiaji wanaolispia (Ultra subscribers) nchini Marekani kwanza, kabla ya kusambaa maeneo mengine duniani.


Hii ni ishara kuwa Google imeamua kutumia kila silaha iliyonayo ili kuhakikisha inabaki kuwa mfalme wa mtandao. Kwa sasa, takwimu zinaonyesha watu bilioni 2 wanatumia huduma zao za AI kila mwezi, na kwa ujio huu wa Gemini 3, vita ya teknolojia ndio kwanza imeanza upya.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.