Imeelezwa kuwa jamii nchini Tanzania bado inahitaji elimu zaidi kuhusu njia bora za kukabiliana na kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, sambamba na elimu ya afya ya uzazi, ili kujenga taifa lililo salama na lenye maadili mema.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Bi. Suzan Cleophos, Ofisa Miradi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Flaviana Matata Foundation (FMF), wakati wa warsha iliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuripoti kwa ufasaha matukio ya unyanyasaji wa kijinsia na kutoa elimu sahihi ya uzazi kwa vijana.
Bi. Suzan alieleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali, taasisi mbalimbali, na FMF, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vinavyowakumba watoto na watu wazima, bado vinaendelea kuripotiwa katika baadhi ya mikoa nchini. Kutokana na hali hiyo, alisisitiza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza juhudi za kutoa elimu ili kukabiliana na tatizo hili kwa nguvu zaidi.
“Elimu bado ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali, taasisi nyingine, na sisi kama FMF, bado kuna maeneo ambako vitendo hivi vinaendelea kutokea. Tunahitaji kushirikiana kwa pamoja na kuendelea kuelimisha jamii ili kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa unyanyasaji huu katika jamii yetu,” alisema Bi. Suzan.
Aliongeza kuwa taasisi ya FMF inaendelea na mipango yake ya kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini, ikishirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wengi zaidi. “Lengo letu siyo tu kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, bali pia kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wetu. Hii ni muhimu sana katika kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni na maambukizi ya magonjwa kama vile VVU,” alifafanua Bi. Suzan.
Alibainisha kuwa mpango huo wa kutoa elimu kwa ajili ya kukomesha unyanyasaji wa kijinsia unaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na mfuko wa 'Woman Fund Trust' (WFT).
Kwa upande wake, Bi. Rehema Longo, mwezeshaji katika warsha hiyo kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, alisema kuwa elimu kama hiyo ina mchango mkubwa katika kukabiliana na tabia zisizofaa katika jamii. “Vijana, hususan wasichana, wanakabiliwa na changamoto nyingi. Elimu kama hii ikiwafikia itawasaidia kuwa na uelewa wa jinsi ya kujikinga na unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuwa na maarifa sahihi kuhusu afya yao ya uzazi,” alisema Bi. Rehema.
Aliongeza: “Kupitia warsha kama hizi kwa wadau ambao ni daraja muhimu la kuifikia jamii, tunafanikiwa sana katika kujenga uelewa. Tunaishukuru na kuipongeza FMF kwa kutambua umuhimu huu wa kutoa elimu kwa vijana na kwa jitihada zao za kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji.”
Inaelezwa kuwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kushirikisha wadau mbalimbali, na kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuripoti masuala haya kwa usahihi ni hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama ambayo inalinda haki za wote, hasa wanawake na watoto.