Biashara au 'Upátu'? OpenAI Yaingia Dili Tata na Mwekezaji Wake, Wachumi Wanusa Harufu ya 'Mzunguko wa Pesa'

it | Wed Dec 03 2025


Biashara au 'Upátu'? OpenAI Yaingia Dili Tata na Mwekezaji Wake, Wachumi Wanusa Harufu ya 'Mzunguko wa Pesa'

Katika ulimwengu wa biashara za kimataifa, kuna msemo usemao "Mkono mtupu haulambwi," lakini kinachoendelea kati ya kampuni ya OpenAI (wamiliki wa ChatGPT) na wafadhili wao wakuu, Thrive Capital, kimezua maswali mazito na minong'ono ya "mchezo wa kuigiza" wa kifedha. OpenAI imetangaza kununua hisa katika kampuni tanzu ya mfadhili wake huyo, hatua ambayo wachumi wameibatiza jina la "Circular Deal" au kwa lugha nyepesi ya mtaani, "Biashara ya Kujizungusha."


Tukio hili la tarehe 1 Desemba (Saa za Marekani) limepokelewa kwa hisia mseto. Wakati OpenAI ikisisitiza kuwa lengo ni kutanua matumizi ya Akili Mnemba (AI) makazini, wakosoaji wanadai huu ni mchezo wa "kupa na kupokea" unaolenga kupandisha thamani ya makampuni hayo kimahesabu tu.


Mchezo wa "Nipe Nikupe"


Kiini cha sakata hili ni uamuzi wa OpenAI kununua hisa (kiasi hakikutajwa) katika kampuni mpya inayoitwa Thrive Holdings, iliyoanzishwa mwezi Aprili na kampuni ya uwekezaji ya Thrive Capital. Kinachofanya jambo hili kuwa la kushangaza ni kwamba Thrive Capital ndiye mwekezaji mkubwa zaidi wa OpenAI.


Wachambuzi wanasema huu ni mzunguko wa pesa uleule: Thrive inampa pesa OpenAI, halafu OpenAI inarudisha sehemu ya pesa hizo kwa Thrive kwa kununua hisa. Ni kama vile kuchota maji kisimani na kuyamwaga humo humo kisimani ili kuonyesha kisima kimejaa.


Hii inakuja huku kukiwa na kumbukumbu kuwa OpenAI imepokea uwekezaji wa kufuru kutoka kwa kampuni ya NVIDIA wa takriban Dola Bilioni 100 (sawa na Shilingi Trilioni 270 za Kitanzania), na kisha kutangaza kuwa itatumia pesa hizo kununua vipuri (GPUs) kutoka kwa huyo huyo NVIDIA. Vilevile, wana mkataba na AMD unaowapa haki ya kununua hisa kwa bei ya kutupa (senti 1).


Wataalamu wa soko la hisa wanaonya kuwa "Mzunguko huu wa Pesa" (Circular Deals) unaweza kutumika kutengeneza picha ya uongo ya ukuaji wa kampuni (Artificial Inflation), jambo ambalo ni hatari kwa uchumi ikiwa puto hilo litapasuka.


Urafiki wa Sam Altman na 'Mshikaji' Wake


Nyuma ya pazia la dili hili kuna urafiki wa "chanda na pete" kati ya Mkurugenzi wa OpenAI, Sam Altman, na Bosi wa Thrive Capital, Joshua Kushner. Ikumbukwe kuwa Kushner ndiye aliyesimama kidete na kuhakikisha Altman anarudi kazini baada ya kufukuzwa kwa muda mwaka 2023. Hivyo, wengi wanaona dili hili kama namna ya kupeana shukrani.


Mpango Mkakati: Kuamsha 'Maiti' za Kibiashara


Licha ya ukosoaji huo, kuna hoja ya kibiashara mezani. Thrive Holdings inanunua kampuni za kizamani za huduma (kama uhasibu na IT) ambazo hazina mvuto. Mpango wa OpenAI ni kuingiza timu zake za wataalamu katika kampuni hizo na kubadilisha mifumo yake kwa kutumia AI.


Akili ni hii: Ikiwa OpenAI itafanikiwa kuzifanya kampuni hizo ziwe na ufanisi kwa kutumia AI, thamani yake itapanda. Kwa kuwa OpenAI inamiliki hisa huko, itapata faida mara mbili—faida ya hisa kupanda na malipo ya huduma za AI.


Joshua Kushner amekaririwa akisema, "Tunafuraha kuleta teknolojia ya kisasa ya OpenAI katika sekta ambazo zina uwezo mkubwa lakini zimebaki nyuma."


Accenture Nayo Yajiunga na Mduara


Katika hatua nyingine, OpenAI imetangaza ushirikiano mpya na kampuni kubwa ya ushauri wa kibiashara duniani, Accenture. Kupitia mpango huu, maelfu ya wafanyakazi wa Accenture wataanza kutumia mfumo wa ChatGPT Enterprise kurahisisha kazi zao.


Kwa wafanyabiashara na wachumi wa Tanzania, sakata hili la OpenAI linatoa funzo muhimu: Katika uchumi wa kisasa wa kidijitali, mipaka kati ya mwekezaji, mteja, na mbia inazidi kufutika. Je, hii ni mbinu mpya ya kukuza mtaji au ni ujanja wa soko? Muda utasema.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.