Upepo wa kisiasa na kibiashara katika ulimwengu wa Akili Mnemba (AI) unabadilika kwa kasi ya ajabu. Katika hatua iliyowashangaza wengi na kutikisa himaya ya OpenAI (wamiliki wa ChatGPT), vigogo wawili wakubwa wa teknolojia duniani, Microsoft na NVIDIA, wametangaza kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa mpinzani mkuu wa OpenAI, kampuni ya Anthropic.
Katika tangazo lililotolewa Novemba 18, Microsoft imeahidi kuwekeza hadi Dola za Kimarekani bilioni 5 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 13), huku NVIDIA ikiweka dau kubwa zaidi la hadi Dola bilioni 10 (takriban TZS Trilioni 26). Jumla ya uwekezaji huu ni zaidi ya bajeti ya nchi nyingi za Afrika, ikiashiria vita mpya ya kutawala soko la AI.
Biashara ya "Nipe Nikupe"
Huu si msaada wa bure; ni biashara ya kimkakati. Kama sehemu ya makubaliano haya:
- Anthropic itatumia kiasi cha Dola bilioni 30 kununua huduma za kompyuta wingu (cloud services) kutoka kwa Microsoft Azure.
- Pia, watanunua miundombinu ya kisasa ya kompyuta kutoka NVIDIA (yenye usanifu wa Grace Blackwell na Vera Rubin) yenye uwezo wa Gigawati 1 (1GW). Wataalamu wanakadiria kuwa mtambo wa ukubwa huu unagharimu kati ya Dola bilioni 20 na 25.
Microsoft Yacheza Pande Zote Mbili
Mkurugenzi wa Microsoft, Satya Nadella, alifafanua hatua hii kwa umakini: "Sisi na Anthropic tutakuwa wateja wa kila mmoja... OpenAI bado ni mshirika wetu muhimu, lakini tunapanua wigo ili kuwa na mfumo imara zaidi."
Kauli hii inatafsiriwa kama mbinu ya Microsoft ya kutotaka kuweka "mayai yake yote kwenye kikapu kimoja" cha OpenAI. Kwa kuwekeza kwa mpinzani, wanajilinda isitokee OpenAI ikayumba au kupata matatizo, biashara yao ya AI isife.
NVIDIA Yabadilisha Gia Angani
Kwa upande wa NVIDIA, hatua hii ni ya kushangaza zaidi. Hivi karibuni, kampuni hiyo ilikuwa na uhusiano mbaya na Anthropic, hasa baada ya Anthropic kuunga mkono vikwazo vya kuuza 'chip' za NVIDIA nchini China. Lakini pesa haina adui. Mkurugenzi wa NVIDIA, Jensen Huang, amesema ushirikiano huu mpya ni "ndoto iliyotimia" na utasaidia kuboresha mfumo wa 'Claude' wa Anthropic.
Hii inaonyesha kuwa NVIDIA nayo inataka kuhakikisha kuwa 'chips' zake zinatumiwa na kila mbabe wa AI, siyo OpenAI pekee (ambayo hivi karibuni imekuwa ikitanua ushirikiano na AMD na Oracle).
Anthropic Yapaa Kithamani
Pamoja na uwekezaji huu mpya kutoka kwa Microsoft na NVIDIA, Anthropic bado imeendelea kumtambua Amazon (AWS) kama mshirika wake mkuu wa kibiashara (ambaye tayari walisaini naye dili la Dola bilioni 38).
Habari hizi zimeipandisha hadhi Anthropic kwa kasi ya roketi. Thamani ya kampuni hiyo sasa inakadiriwa kufikia Dola bilioni 350 (TZS Trilioni 910), ikiwa imepanda mara mbili kutoka Dola bilioni 183 mwezi Septemba. Hii inaisogeza karibu sana na thamani ya OpenAI iliyo kwenye Dola bilioni 500.
Wachambuzi wa soko, kama Gil Luria, wanasema huu ni mkakati wa wazi wa "De-OpenAI-zation"—yaani kupunguza utegemezi kwa kampuni moja na kuimarisha ushindani, jambo ambalo litakuwa na faida kubwa kwa ukuaji wa teknolojia hii duniani.