Wakati dunia ikishangilia maendeleo ya Akili Mnemba (AI), nchini Marekani, ndoto za vijana wengi wa Kizazi Z (waliozaliwa kati ya 1997-2012) zinayeyuka kutokana na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira unaosababishwa moja kwa moja na teknolojia hiyo. Hali hii imeanza kuzua mjadala mzito wa kisiasa kuhusu mustakabali wa ajira katika ulimwengu unaoongozwa na mashine.
Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha picha ya kutisha. Kiwango cha jumla cha ukosefu wa ajira nchini Marekani kilifikia asilimia 4.3 mwezi Agosti, kiwango kibaya zaidi katika miaka minne. Hata hivyo, janga hili linawaathiri zaidi wahitimu wapya wa vyuo vikuu. Takwimu za Benki Kuu ya New York zinaonyesha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 22-27 ulipanda hadi asilimia 5.8, juu zaidi ya wastani wa kitaifa. Wachambuzi wanasema hii si dalili ya mdororo wa kiuchumi, bali ni matokeo ya moja kwa moja ya kampuni kuachana na ajira za wanadamu na kukumbatia mifumo ya AI.
Tangu kuzinduliwa kwa ChatGPT mwishoni mwa 2022, kasi ya matumizi ya AI imeongezeka maradufu. Kazi za ofisini zilizokuwa zikihitaji wahitimu wapya kama uhasibu, sheria, huduma kwa wateja, na usimamizi wa nyaraka sasa zinafanywa na programu za kompyuta. Hata sekta ya teknolojia, ambayo ilikuwa tegemeo la ajira, imeanza kupunguza nafasi za kazi za watengeneza programu wa ngazi ya chini, kwani AI inaweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Hali hii imeingia katika medani ya siasa. Rais Donald Trump amependekeza mkakati wa kupunguza fedha kwa vyuo vikuu na badala yake kuwekeza katika vyuo vya ufundi (blue-collar), akisema mustakabali upo kwa mafundi kama umeme na bomba. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mkakati huu hautoshi, kwani hata kazi za ufundi wa kisasa kama utengenezaji wa roboti na betri zinahitaji maarifa ya hali ya juu.
Ndani ya chama cha Democratic, kuna mgawanyiko. Baadhi wanataka sheria za kudhibiti AI, lakini wakilenga zaidi masuala ya kimaadili. Wengine, wenye mrengo wa kimaendeleo, wanapendekeza suluhu kali zaidi kama Serikali kutoa "Mshahara wa Msingi kwa Wote" (Basic Income) au kutaifisha baadhi ya sekta muhimu ili kuhakikisha wananchi wanaishi vizuri hata bila ajira.
Suala la ajira linatarajiwa kuwa agenda kuu katika chaguzi zijazo za 2026 na 2028, huku Kizazi Z, ambacho sasa kinahangaika na maisha, kikitafuta mwanasiasa atakayetoa suluhu ya kweli kwa changamoto hii mpya.