Zelenskyy Ajaribu Kurekebisha Mahusiano na Marekani Baada ya Mvutano na Trump

international | Mon Mar 03 2025


Zelenskyy Ajaribu Kurekebisha Mahusiano na Marekani Baada ya Mvutano na Trump

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema kuwa nchi yake iko tayari kusaini makubaliano ya madini na Marekani, akionyesha matumaini kuwa Washington pia iko tayari kwa hatua hiyo. Kauli hii inatafsiriwa kama juhudi za kupunguza mvutano uliotokea baada ya mkutano wake wenye utata na Rais wa Marekani, Donald Trump, wiki iliyopita.


Akizungumza mnamo Machi 2 baada ya kushiriki katika mkutano wa dharura wa viongozi wa Ulaya mjini London, Zelenskyy alisisitiza kuwa uhusiano kati ya Ukraine na Marekani utaendelea licha ya changamoto zilizojitokeza. "Nadhani uhusiano wetu utaendelea. Tunapaswa kutazama mbele," alisema katika mkutano na waandishi wa habari.


Kuhusu mvutano wake na Trump mnamo Februari 28, ambapo mazungumzo yao yalirushwa mubashara na kuibua sintofahamu kimataifa, Zelenskyy alisema, "Sidhani kama ni sahihi mazungumzo ya aina hiyo kuwa hadharani kabisa. Hali hiyo haileti chochote chanya kwa ushirikiano wetu."


Mvutano huo ulianza wakati Zelenskyy aliposisitiza kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, haaminiki na hivyo akaomba Marekani kutoa dhamana zaidi za kiusalama kwa Ukraine. Trump alijibu kwa ukali, akisema kuwa Ukraine haipaswi kudai msaada wa Marekani bila shukrani, akiongeza kuwa bila msaada wa Washington, "Ukraine ingekuwa imeanguka ndani ya wiki mbili."


Trump aliendelea kumshutumu Zelenskyy kwa kupinga mapendekezo yake ya kumaliza vita na Urusi, akidai kuwa rais huyo wa Ukraine anaendesha "mchezo wa hatari" unaoweza kusababisha Vita vya Tatu vya Dunia. Alionya kuwa Marekani inaweza kujiondoa kwenye mgogoro wa Ukraine, akisema, "Unakubaliana au la. Tusipokubaliana, sisi tutajiondoa, na utabaki peke yako katika vita hivi."


Matamshi ya Zelenskyy kuhusu utayari wa kusaini makubaliano ya madini yanaonekana kuwa hatua ya kutuliza hali baada ya mazungumzo hayo makali. Hata hivyo, utawala wa Trump umeendelea kumuandama Zelenskyy, ukimtaka abadili msimamo wake kuhusu vita na hata kupendekeza mabadiliko ya uongozi nchini Ukraine.


Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Mike Waltz, aliambia CNN kuwa "tunahitaji kiongozi wa Ukraine ambaye anaweza kufanya mazungumzo na Marekani na hatimaye na Urusi ili kumaliza vita hivi."


Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Mike Johnson, naye aliongeza shinikizo dhidi ya Zelenskyy kwa kusema, "Lazima kuwe na mabadiliko. Zelenskyy ama abadili mtazamo wake na arejee kwenye meza ya mazungumzo akiwa na shukrani, au mtu mwingine achukue nafasi yake kuiongoza Ukraine."


Licha ya shinikizo hili, Zelenskyy alisema kuwa hana matarajio kuwa Marekani itasitisha msaada wake kwa Ukraine lakini akaongeza kuwa nchi yake inaendelea kujiandaa kwa hali yoyote itakayojitokeza.


Hali hii inaonyesha mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi wa Ukraine na Marekani juu ya jinsi ya kushughulikia vita dhidi ya Urusi, huku Washington ikiweka wazi kuwa uvumilivu wake kwa serikali ya Zelenskyy unapungua.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.