Rais wa Marekani, Donald Trump, anafikiria mpango wa kuwahamisha wanajeshi wa Marekani waliopo nchini Ujerumani hadi nchi nyingine za Ulaya Mashariki, huku Hungaria ikitajwa kuwa chaguo linalozingatiwa zaidi.
Kwa mujibu wa The Telegraph, chanzo kilicho karibu na Ikulu ya White House kilifichua kuwa Trump amekerwa na jinsi mataifa ya Ulaya yanavyoendelea kushinikiza msaada wa kijeshi kwa Ukraine, wakati Marekani inajaribu kufanya mazungumzo ya amani na Urusi.
Kwa sasa, kuna takriban wanajeshi wa Marekani 35,000 waliopo Ujerumani, na mpango wa kuwaondoa unahusiana na msimamo wa Trump wa kupunguza mzigo wa Marekani katika ulinzi wa Ulaya, hasa kwa mataifa ambayo anaona kuwa hayatoi mchango wa kutosha katika juhudi za kijeshi.
Hungaria: Kituo Kipya cha Wanajeshi wa Marekani?
Hungaria inatajwa kuwa kituo kinachofaa kwa sababu kadhaa. Ingawa ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na NATO, nchi hiyo imekuwa na msimamo tofauti na mataifa mengi ya Magharibi, hasa chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Viktor Orbán.
Orbán, ambaye mara nyingi amepewa jina la “Trump wa Ulaya”, amekuwa akizuia baadhi ya maamuzi ya EU na NATO kuhusu vita vya Ukraine. Hungaria imeonyesha mwelekeo wa kuunga mkono Urusi kwa kiwango fulani, jambo lililoonekana wazi katika mkutano wa kilele wa EU mnamo Machi 6, ambapo ilikataa kushiriki katika azimio la pamoja la kusaidia Ukraine kijeshi.
Marekani na Mvutano wa Kijeshi Ulaya
Hatua ya Trump inarejesha kumbukumbu ya uamuzi wake wa kwanza wa urais (2017-2021), ambapo aliamua kuondoa wanajeshi 12,000 kutoka Ujerumani, kabla ya mpango huo kufutwa na serikali ya Joe Biden.
Katika kujibu tetesi za mpango huu mpya wa Trump, msemaji wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani (NSC), Brian Hughes, alisema kuwa “Hakuna tangazo lolote rasmi lililo tayari kutolewa kwa sasa”. Hata hivyo, aliongeza kuwa Marekani daima hupitia upya usambazaji wa vikosi vyake vya kijeshi ili kukabiliana na vitisho vya sasa na kulinda maslahi yake kimataifa.
Ikiwa mpango huu wa Trump utaendelea, basi huenda ukazidisha mgawanyiko kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya, hasa katika kipindi ambacho vita vya Ukraine vinaendelea na mahusiano ya kimataifa yanazidi kuwa tete.