Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amelishauri Jeshi la Polisi la Tanzania kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu mahali walipo wanahabari wawili – Boniface Mwangi kutoka Kenya na Agatha Atuhaire wa Uganda. Wakili Olengurumwa amesema kuwa ukimya unaendelea kuzunguka suala hili unaweza kusababisha taharuki na maneno yasiyo ya lazima, ambayo yanaweza kuharibu sifa ya Tanzania kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 21, 2025, jijini Dar es Salaam, Wakili Olengurumwa alieleza kuwa tangu Mei 18, kumekuwa na ripoti za kukamatwa na kushikiliwa kwa wanahabari hao katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini. Alisema kuwa ukimya huu unakiuka taratibu za kisheria za haki za binadamu, kwani sheria inataka kila mtu anayeshikiliwa kizuizini apewe haki ya kupata msaada wa kisheria na kufikishwa mahakamani kwa wakati unaofaa.
“Sheria zetu za nchi na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu zinaelekeza wazi kuwa haki za watu waliokamatwa na kushikiliwa zinapaswa kuheshimiwa. Hata kama wanahabari hawa wana tuhuma zinazowakabili, ni muhimu kwa taratibu za kisheria kufuatwa. Ikiwa hawatafikishwa mahakamani, basi wanapaswa kurudishwa katika nchi zao kwa heshima,” alisisitiza Wakili Olengurumwa.
Aliongeza kuwa mnamo Mei 20, 2025, zilisambaa taarifa ambazo zilidai kuwa wanahabari hao walisharudishwa katika nchi zao. Hata hivyo, baada ya kufuatilia kwa karibu, ilibainika kuwa hawakurudishwa, hali ambayo inaongeza mkanganyiko na kutoa mashaka kuhusu utendaji wa taasisi za dola.
Wakili Olengurumwa pia alizungumzia kuhusu madai ya kukiukwa kwa haki za msingi za wanahabari hao. Alibainisha kuwa kitendo cha kuzuia mawakili wao kuonana nao ni ukiukwaji wa wazi wa haki za msingi. Alionya kuwa hali hii inaharibu taswira ya Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na inaweza kuleta picha kuwa nchi haizingatii misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu.
“Kitendo hiki cha kuzuia mawakili kuonana na wateja wao kinajenga picha mbaya sana nje ya nchi yetu. Tunasihi mamlaka husika kutumia busara katika kumaliza suala hili bila kulidhalilisha taifa letu,” aliongeza Wakili Olengurumwa.
Alionya zaidi kuwa endapo Jeshi la Polisi halitachukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria, THRDC itapeleka maombi rasmi mahakamani ili mahakama iamuru mamlaka husika kutoa taarifa au kuelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Alieleza kuwa usiri unaoendelea unaweza kuwa na madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na kuibuka kwa madai ya mateso dhidi ya wanahabari hao. Alisisitiza kuwa hali kama hiyo haifai kutokea kwa wageni walioko nchini Tanzania.
Katika taarifa yake iliyotolewa Mei 19, 2025, THRDC ilitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuheshimu viwango vya kimataifa vinavyolinda haki za binadamu, hasa kwa watu wanaoshikiliwa kizuizini. Shirika hilo lilisistiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa haki za wanahabari hao zinalindwa na kwamba wanatendewa kwa mujibu wa sheria.