Kampuni kubwa ya teknolojia duniani, Microsoft, imetangaza kusitisha utoaji wa huduma zake muhimu za kidijitali kwa kitengo maalum cha jeshi la Israel. Uamuzi huu umekuja kufuatia ripoti za uchunguzi zilizodai kuwa teknolojia ya kampuni hiyo ilikuwa ikitumika kufanya ujasusi wa kina dhidi ya raia wa Kipalestina.
Katika barua pepe kwa wafanyakazi, Rais wa Microsoft, Brad Smith, alithibitisha kwamba kampuni yake imewaarifu maafisa wa ulinzi wa Israel kuhusu kusitishwa kwa huduma za kuhifadhi data mtandaoni (cloud) na zile za akili bandia (AI).
Hatua hii kali inafuatia ripoti iliyochapishwa mwezi uliopita na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza. Ripoti hiyo ilifichua kuwa kitengo cha ujasusi cha jeshi la Israel, kinachojulikana kama ‘Unit 8200’, kimekuwa kikitumia mfumo wa ‘cloud’ wa Microsoft unaoitwa Azure kujenga hifadhidata kubwa. Hifadhidata hiyo ilidaiwa kuhifadhi mamilioni ya rekodi za mazungumzo ya simu za Wapalestina katika maeneo ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi. Taarifa hizo za siri zilitumika kupanga mashambulizi ya angani na operesheni nyingine za kijeshi.
Kufuatia madai hayo mazito, Microsoft ilianzisha uchunguzi wake wa ndani. Matokeo ya awali yanaonekana kuthibitisha sehemu ya tuhuma hizo. Brad Smith alisema, "Ingawa uchunguzi bado unaendelea, tumepata ushahidi unaounga mkono baadhi ya madai ya The Guardian. Ushahidi huu unahusisha matumizi ya hifadhi ya Azure na huduma za AI yaliyofanyika nchini Uholanzi."
Hii inamaanisha teknolojia ya kampuni kubwa ya Marekani ilitumiwa na jeshi la Israel kufanya ufuatiliaji mkubwa dhidi ya Wapalestina na kutumika kama silaha katika mzozo unaoendelea.
Suala hili pia limezua mzozo ndani ya Microsoft. Hivi karibuni, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo waliandamana kupinga matumizi ya programu zao katika uvamizi wa Israel huko Gaza, hatua iliyosababisha wafanyakazi watano kufukuzwa kazi.
Hata hivyo, Rais Smith alisisitiza kuwa wakati wa uchunguzi, kampuni haikuangalia data za wateja wake ili kulinda faragha. Alisema, "Sote tuna jukumu la kulinda faragha. Hii ndiyo inajenga imani ya wateja wetu na kuleta thamani katika biashara yetu."