Mvutano unaotokana na vita vya Gaza umeingia ndani ya ofisi za makampuni makubwa ya teknolojia duniani (Big Tech) huko Silicon Valley, na kusababisha mgawanyiko mkubwa. Makampuni haya, ambayo awali yalikuwa na sifa ya kuruhusu uhuru wa wafanyakazi kutoa maoni yao ya kisiasa, sasa yanaonekana kuchukua hatua kali dhidi ya maandamano na kauli zozote zinazohusiana na mzozo wa Gaza, hasa zile zinazoikosoa Israel.
Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, kampuni ya Microsoft imewafuta kazi wafanyakazi wawili walioshiriki maandamano. Mmoja wa wafanyakazi hao alitundika bendera ya Palestina nje ya makao makuu ya kampuni, huku mwingine akishiriki katika kuikalia ofisi ya mmoja wa viongozi wa juu wa kampuni hiyo. Hii ni ishara ya msimamo mpya mkali ndani ya kampuni hiyo.
Uchunguzi wa ndani wa nyaraka za kampuni uliofanywa na gazeti hilo umebaini kuwa Microsoft imekuwa ikifuta mara kwa mara maoni ya wafanyakazi kwenye majukwaa yake ya ndani yanayohusu mateso ya raia huko Gaza. Katika tukio moja, mfanyakazi aliyeandika kuhusu "uhaba wa chakula na madhara ya mashambulizi" kwa wakazi wa Gaza, aliona ujumbe wake ukiondolewa huku msimamizi akimtaka "kuzingatia miongozo ya jamii."
Akijibu madai kuwa teknolojia ya Microsoft inatumika katika mashambulizi Gaza, Rais wa kampuni hiyo, Brad Smith, alisema kampuni "inachunguza madai hayo" lakini akaongeza kuwa "uchunguzi wa awali wa madai kama hayo haukupata ushahidi wowote." Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi waliofutwa, Abdo Muhammad, alidai kuwa "kampuni imekuwa ikijaribu kupuuza kila mara wafanyakazi wanapouliza maswali kuhusu ushirikiano wake na Israel."
Hali kama hiyo inashuhudiwa pia katika kampuni ya Google, ambapo mgogoro umekuwa mkubwa zaidi. Mwezi Aprili mwaka jana, Google iliwafuta kazi wafanyakazi 28 waliofanya maandamano ya kukalia ofisi wakipinga mkataba wa huduma za "cloud" wenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 1.2 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania trilioni 3.12) na serikali ya Israel. Siku chache baadaye, wafanyakazi wengine 20 walifukuzwa.
Google sasa imeweka sheria kali zaidi kwenye majukwaa yake ya ndani. Matumizi ya neno "genocide" (mauaji ya kimbari) katika barua pepe au mijadala ya ndani yanasababisha ujumbe kufutwa mara moja. Msimamo rasmi wa kampuni ni kwamba "mahali pa kazi si mahali pa mijadala ya kisiasa, na ujumbe unaoleta usumbufu kwa kazi utaondolewa." Hii ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2018, ambapo maandamano ya wafanyakazi yalilazimisha Google kujiondoa kwenye mradi wa akili mnemba (AI) na Wizara ya Ulinzi ya Marekani. Sasa, inaonekana makampuni haya yamechagua kulinda mikataba yao mikubwa na serikali badala ya kuruhusu uhuru wa maoni ya wafanyakazi wao.