Microsoft Yazindua 'Chip' Mpya ya Cobalt 200 yenye Kasi ya Kufuru

it | Thu Nov 20 2025


Microsoft Yazindua 'Chip' Mpya ya Cobalt 200 yenye Kasi ya Kufuru

Katika vita vya kuwania utawala wa teknolojia ya kuhifadhi taarifa mtandaoni (Cloud Computing), kampuni ya Microsoft imeamua kuonyesha misuli yake kwa kuzindua "ubongo" mpya kabisa wa kuendesha seva zake. Katika mkutano wao mkubwa wa mwaka wa 'Microsoft Ignite' uliomalizika hivi punde, kampuni hiyo imetambulisha rasmi 'chip' yake mpya iitwayo Azure Cobalt 200.


Hii siyo chip ya kawaida unayoweza kuikuta kwenye kompyuta ya mkononi dukani Kariakoo; ni mtambo maalum ulioundwa kusukuma mzigo mzito wa data katika vituo vikuu vya kuhifadhi taarifa duniani.


Nguvu Maradufu, Umeme Kidogo


Cobalt 200 ni mrithi wa toleo la kwanza (Cobalt 100) lililotoka miaka miwili iliyopita. Microsoft inajigamba kuwa toleo hili jipya lina kasi na uwezo mkubwa kwa asilimia 50 zaidi kuliko kaka yake wa zamani.


Siri ya nguvu hii iko wapi? Microsoft wameishirikisha kampuni ya kutengeneza 'chip' ya Taiwan (TSMC) kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ya '3-nanometer'. Kwa lugha nyepesi, teknolojia hii inaruhusu kuweka nguvu kubwa ya kiutendaji kwenye kifaa kidogo, huku ikitumia umeme kidogo sana. Hii ni habari njema kwa kampuni zinazohangaika kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA.


Ubunifu wa Kijanja


Microsoft hawakukurupuka. Kabla ya kuunda Cobalt 200, walifanya 'simulation' (majaribio ya kidijitali) zaidi ya 2,800 wakitumia data halisi za wateja wao. Walipima michanganyiko tofauti ya kiufundi wapatao 350,000 kabla ya kupata muundo huu bora zaidi.


Ndani ya 'chip' hii moja kuna 'cores' 132 zinazofanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu. Imetengenezwa kwa kutumia usanifu wa ARM Neoverse V3, jambo linaloifanya iwe na uwezo wa kipekee wa kubadilisha matumizi ya umeme kulingana na ukubwa wa kazi (workload). Ikiwa kazi ni ndogo, inapunguza nguvu ili kuokoa umeme; kazi ikiongezeka, inaongeza kasi papo hapo.


Usalama Kama Ikulu


Katika ulimwengu wa sasa ambapo udukuzi wa data umekuwa janga, Microsoft wameweka ulinzi mkali ndani ya Cobalt 200. Wametumia teknolojia ya Confidential Compute Architecture (CCA) ambayo inahakikisha kuwa kumbukumbu (memory) ya kompyuta imejitenga kabisa na mfumo wa uendeshaji. Hii ina maana kwamba hata kama mdukuzi atafanikiwa kuingia kwenye 'server', hawezi kusoma data zilizoko kwenye 'memory' kwa sababu zimefungwa (encrypted) kwa kiwango cha juu cha kijeshi (FIPS 140-3 Level 3).


Kasi Kwenye Kazi Maalum


Kitu kingine cha kuvutia ni jinsi walivyotatua tatizo la 'foleni' za data. Wameongeza vipande maalum (custom silicon blocks) ndani ya chip hiyo ambavyo kazi yake ni moja tu: kufunga na kufungua mafaili (compression & decompression) na kusimamia usimbaji (encryption). Kwa kuondoa kazi hizi ndogondogo kwenye CPU kuu, wameruhusu 'ubongo' mkuu wa chip hiyo ujikite kwenye kazi nzito za kibiashara, kama vile kuendesha kanzi data za Azure SQL kwa ufanisi zaidi.


Lini Itapatikana?


Tayari Microsoft wameanza kutumia 'chip' hizi kwenye vituo vyao vya data kwa majaribio ya ndani. Hata hivyo, kwa makampuni na mashirika makubwa (ikiwemo yale ya hapa Tanzania yanayotumia huduma za Azure), teknolojia hii itaanza kupatikana rasmi mwaka 2026. Hii ni hatua kubwa kwa Microsoft katika kuhakikisha kuwa hawaachwi nyuma na washindani wao kama Amazon (AWS) na Google katika vita ya kutoa huduma bora na za haraka za 'cloud'.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.