Simanzi Nzito Hong Kong: Watu 83 Wateketea kwa Moto, Mamia Wengine Hawajulikani Walipo

international | Fri Nov 28 2025


Simanzi Nzito Hong Kong: Watu 83 Wateketea kwa Moto, Mamia Wengine Hawajulikani Walipo

Jijini Hong Kong, anga limegubikwa na wingu la moshi mweusi na vilio vya "kusaga meno" baada ya janga kubwa la moto kutokea na kuacha maafa ambayo hayajashuhudiwa katika kipindi cha takriban miongo nane. Tukio hili la kusikitisha lilitokea tarehe 26 Novemba 2025, katika eneo la Tai Po, kaskazini mwa Hong Kong, ambapo makazi ya ghorofa ya Wang Fuk Court yaligeuka kuwa tanuru la moto.


Hadi kufikia sasa, imethibitishwa kuwa watu 83 wamepoteza maisha katika mkasa huo, huku wengine 76 wakiwa wamejeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini. Hata hivyo, hofu kubwa imetanda juu ya hatima ya watu 279 ambao bado wameorodheshwa kama "watu wasiojulikana walipo" (missing persons), huku ndugu na jamaa wakikesha kwenye vituo vya uokoaji wakisubiri habari njema au mbaya.


Moto Uliosambaa Kama Njuka

Moto huo haukuwa wa kawaida. Katika hali ya kushangaza na kutisha, ndimi za moto ziliweza kuruka na kuunguza majengo saba kati ya nane yanayounda "estate" hiyo kubwa. Eneo hili ni makazi ya watu wengi, likiwa na takriban kaya 2,000 na jumla ya wakazi wapatao 4,800.


Mashuhuda wanaeleza kuwa kasi ya moto huo ilichangiwa na vifaa vya ujenzi vilivyokuwa vikitumika kwa ajili ya ukarabati. Hong Kong ni maarufu kwa kutumia 'Mianzi' (Bamboo scaffolding) kujenga au kukarabati maghorofa marefu badala ya vyuma tunavyoona hapa Tanzania. Mianzi hiyo, pamoja na madirisha yaliyokuwa yamefunikwa na 'polystyrene' (aina ya plastiki nyepesi), viligeuka kuwa kichocheo cha moto huo kusambaa kwa kasi ya ajabu na kufanya zoezi la uokoaji kuwa ngumu.


Bei Chee Yagharimu Maisha

Ingawa nyumba hizi za Wang Fuk Court zilijengwa kwa ajili ya kusaidia wananchi wa kipato cha chini kupata makazi nafuu, imebainika kuwa "bei chee ni ghali." Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mifumo ya usalama ilikuwa duni au haifanyi kazi kabisa.


Inaripotiwa kuwa ving'ora vya moto (fire alarms) vilikaa kimya wakati janga likianza, na mabomba ya maji ya dharura (fire hydrants) hayakutoa ushirikiano. Mbaya zaidi, mfumo wa 'sprinklers' (vinyunyizio vya maji vya ndani) ulikuwa haba, jambo lililofanya iwe vigumu kwa wakazi kudhibiti moto huo katika hatua za awali kabla ya kusambaa. Hii imeamsha hasira kali kwa umma, wakihoji inakuwaje usalama wa raia wa kipato cha chini unapuuzwa kiasi hicho.


Jitihada za Uokoaji na Hatua za Serikali

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Hong Kong limeweka kambi eneo la tukio, huku zaidi ya askari 1,200 na magari ya kuzima moto 196 yakishiriki katika operesheni hiyo ambayo inaelezwa kuwa ngumu kutokana na ukubwa wa majengo na moshi mzito.


Serikali ya Hong Kong, ikionekana kushtushwa na ukubwa wa janga hili ambalo linatajwa kuwa baya zaidi kutokea katika miaka 77 iliyopita, imetangaza hatua za haraka. Mbali na kutoa "kifuta jasho" na misaada ya kibinadamu kwa waathirika, serikali imetangaza kupitia upya matumizi ya mianzi (bamboo scaffolding) katika ujenzi wa maghorofa ili kuzuia majanga kama haya yasijirudie.


Wakati wakazi waliokolewa wakiwa wamehifadhiwa katika vituo vya muda, hali ya sintofahamu bado ni kubwa. Hasira za wananchi zimepanda, wakilaumu mamlaka kwa uzembe wa kutosimamia viwango vya usalama, jambo ambalo limegeuza makazi yao kuwa makaburi.


Tukio hili ni funzo kubwa kwa mataifa yanayoendelea, ikiwemo Tanzania, juu ya umuhimu wa kuzingatia viwango vya usalama katika majengo marefu, hasa yale yanayohudumia watu wengi, ili kuepuka majanga yanayoweza kuzuilika.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.