Wakati Baraza la Mawaziri la Israel likijiandaa kupiga kura kuidhinisha makubaliano ya kihistoria ya kusitisha vita na Hamas, Serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imejikuta katika hatari ya kuporomoka kufuatia upinzani mkali kutoka kwa mawaziri wenye msimamo mkali ndani ya serikali yake ya mseto. Mawaziri hao wamepinga vikali mpango huo wa amani uliosimamiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, wakitishia kujiondoa serikalini endapo utapitishwa.
Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Taifa na kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Otzma Yehudit, alikuwa wa kwanza kuweka wazi msimamo wake. "Siwezi kupiga kura kuunga mkono mkataba unaowaachia huru magaidi wauaji," alisema Ben-Gvir. Alionya vikali kwamba, "Endapo utawala wa Hamas huko Gaza hautasambaratishwa kikamilifu, chama cha Otzma Yehudit kitaiangusha serikali hii ya mseto."
Kauli kama hiyo ilitolewa na Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha na kiongozi wa chama cha Religious Zionist. "Siwezi kushiriki katika sherehe hizi za muda mfupi au kupiga kura kuunga mkono makubaliano haya," alisema Smotrich. Aliongeza kuwa ana "hofu kubwa" juu ya matokeo ya kuwaachia huru "kizazi kijacho cha viongozi wa kigaidi watakaomwaga damu ya Wayahudi." Alisisitiza kuwa Israel inapaswa kuendelea na vita hadi itakapoliangamiza kabisa kundi la Hamas.
Kwa mujibu wa gazeti la Times of Israel, endapo vyama hivyo viwili vitajiondoa, serikali ya Netanyahu itapoteza wingi wake wa viti Bungeni (Knesset). Itabaki na viti 47 tu kati ya 120, hali itakayoweza kusababisha kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema.
Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, vyama vya upinzani vimeahidi kumpa Netanyahu "wigo wa usalama wa kisiasa." Vimesema vitaiunga mkono serikali ili isiporomoke, mradi tu mpango wa amani wa Rais Trump unaendelea kutekelezwa.
Baraza la mawaziri la Israel lilianza kikao chake cha kuidhinisha mkataba huo baada ya kuchelewa kwa saa tatu. Chini ya makubaliano hayo, Hamas itaachia mateka wote (wanaokadiriwa kuwa 20 walio hai na wengine waliofariki) ili Israel iwaachie wafungwa 250 wa Kipalestina wanaotumikia vifungo vya maisha na wengine 1,700 waliokamatwa tangu Oktoba 7, 2023.