Nchi ya Slovenia, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), imechukua hatua ya kihistoria na ya kushangaza kwa kuwa nchi ya kwanza ndani ya Umoja huo kupiga marufuku kabisa biashara ya silaha na Israel. Uamuzi huu umetolewa na Serikali ya Slovenia baada ya kueleza masikitiko yake kuhusu mzozo wa kibinadamu huko Gaza na kile walichokiita kuwa ni kizuizi cha makusudi cha Israel kwa msaada wa kibinadamu.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka kituo cha habari cha Euro News, Serikali ya Slovenia imetangaza kuwa inasitisha mara moja uagizaji wa silaha kutoka Israel, usafirishaji wa silaha kwenda Israel, na hata usafirishaji wa silaha zozote za Israel kupitia ardhi yake. Serikali imetoa taarifa kali ikisema: “Watu wa Gaza wanakufa kutokana na kizuizi cha utaratibu wa misaada ya kibinadamu… wanakufa katika magofu bila maji, chakula, na huduma za msingi za matibabu, na Israel inazuia kwa makusudi hali za msingi za kuishi.”
Serikali ya Slovenia pia imeeleza waziwazi kutoridhishwa kwake na EU, ikisema kuwa Umoja huo umeshindwa kutoa msimamo mmoja kuhusu mzozo wa Israel. Waziri Mkuu wa Slovenia, Robert Golob, alikuwa ametoa onyo mapema kwamba ikiwa EU isingetoa majibu ya kuridhisha hadi katikati ya Julai, nchi yake ingechukua hatua yenyewe. “Kutokana na kutokubaliana kwa ndani na mgawanyiko, EU haiwezi kutekeleza majukumu yake. Kama nchi inayowajibika, tuna wajibu wa kuwa mbele ya wengine,” ilisema taarifa ya Serikali.
Hatua hii ya kupiga marufuku silaha ni mwendelezo wa msimamo mkali ambao Slovenia imekuwa ikichukua dhidi ya Israel. Mwezi Juni mwaka jana, Bunge la Slovenia lilitambua rasmi Palestina kama taifa, likifuata nyayo za Hispania, Ireland, na Norway. Mwezi uliopita, Slovenia pia ilikuwa nchi ya kwanza ya EU kuwakataza kuingia nchini humo mawaziri wawili wa Israel, Bezalel Smotrich na Itamar Ben-Gvir, ikiwataja kuwa "persona non grata" (watu wasiohitajika).
Hata hivyo, waangalizi wa mambo wanaamini kuwa biashara ya silaha kati ya Slovenia na Israel haikuwa kubwa, hivyo uamuzi huu hautakuwa na athari kubwa za kiuchumi kwa pande zote mbili. Badala yake, hatua hii inatazamwa zaidi kama ishara ya kidiplomasia ya kuweka shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel, ikisisitiza umuhimu wa sheria za kimataifa na heshima kwa haki za binadamu.