Serikali ya kijeshi ya Guinea imetangaza uamuzi mzito wa kufuta leseni ya uchimbaji madini ya kampuni ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), uamuzi ambao umeleta sintofahamu kubwa katika sekta ya madini nchini humo. Kitendo hiki kinakuja huku serikali za kijeshi katika ukanda wa Afrika Magharibi zikizidi kuimarisha udhibiti wao kwa rasilimali za asili.
Kupitia hotuba iliyotangazwa na televisheni ya taifa, kiongozi wa kijeshi na Rais wa muda wa Guinea, Kanali Mamady Doumbouya, alitangaza rasmi kwamba kampuni ya Guinea Alumina Corporation (GAC) imeondolewa leseni yake. GAC, ambayo ni kampuni tanzu ya shirika kubwa la kimataifa la Emirates Global Aluminium (EGA) la UAE, ilikuwa ikiendesha moja ya migodi mikubwa ya madini ya bauxite katika mkoa wa Boké kaskazini-magharibi mwa Guinea. Madini ya bauxite ni malighafi muhimu kwa ajili ya kutengeneza alumini.
Leseni hiyo iliyofutwa imekabidhiwa kwa kampuni mpya ya umma iitwayo Nimba Mining Company, ambayo inasimamiwa na Wizara ya Madini na Jiolojia. Ingawa serikali ya kijeshi ilitoa sababu za uvunjaji wa sheria za madini, haikutoa maelezo ya kina ya makosa yaliyofanywa na GAC.
GAC imetoa upinzani mkali dhidi ya uamuzi huo, ikisema kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mkataba wao na sheria za Guinea. Kampuni hiyo ilidai kuwa hatua hii itaweka hatarini ajira za watu zaidi ya 3,000 na inazua maswali mazito juu ya utawala wa sheria nchini humo.
Uongozi wa Guinea ulichukuliwa na Kanali Doumbouya baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Septemba 2021, yaliyomuondoa madarakani Rais Alpha Condé. Tangu alipoingia madarakani, Doumbouya ameonyesha nia ya kuimarisha udhibiti wa serikali kwenye sekta ya madini yenye faida kubwa, akitumia mamlaka yake kuleta mabadiliko makubwa. Hali hii pia inaonekana katika nchi nyingine za Afrika Magharibi zenye serikali za kijeshi kama vile Niger, Burkina Faso na Mali, ambazo zimekuwa zikizidisha shinikizo kwa makampuni ya kigeni ya madini. Kwa mfano, mwezi Juni, serikali ya Niger ilitaifisha kampuni ya Orano, ambayo ni kampuni ya nyuklia ya Ufaransa, huku serikali ya Mali ikiweka mgodi wa dhahabu chini ya usimamizi wake. Hali hii inaweza kuwa funzo kwa nchi za Afrika kama Tanzania, kuwa na mikakati madhubuti ya kusimamia rasilimali zake za asili.