Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amelazimika kurejea nyumbani akiwa mikono mitupu baada ya safari ndefu na iliyosubiriwa kwa hamu nchini Marekani, bila kufanikiwa kupata matokeo yoyote muhimu aliyoyatarajia. Lengo lake kuu la kujadili suala la ushuru wa forodha halikufua dafu, na badala yake alijikuta akikabiliwa na taarifa za Marekani kuwa na mazungumzo na mataifa ambayo ni hasimu au yana uhasiano mbaya na Israel, kama vile Iran na Uturuki. Vyombo vya habari nchini Israel vimeonyesha kukatishwa tamaa kukubwa.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alipokutana na Netanyahu katika Ikulu ya White House, alijibu swali la waandishi kuhusu uwezekano wa kupunguza ushuru wa pande zote kwa Israel kwa kusema, "Pengine siyo," na kuongeza, "Tunazungumzia makubaliano mapya kabisa." Trump alikumbushia msaada mkubwa ambao Marekani inaipatia Israel, akisema, "Tunaipatia Israel dola bilioni 4 (takriban TZS Trilioni 10.4) kwa mwaka. Ni kiasi kikubwa kuliko tunachompa yeyote." Hii ilikuwa ni baada ya Marekani kutangaza hivi karibuni ushuru wa asilimia 17 kwa bidhaa kutoka Israel chini ya mfumo mpya wa ushuru wa pande zote.
Hata hatua ya Israel kujishusha na kutangaza kuondoa mara moja ushuru wake wote kwa bidhaa za chakula na kilimo kutoka Marekani haikuzaa matunda. Ingawa Netanyahu alithibitisha kuwa Israel "itaondoa ushuru huo haraka," na Trump akajibu, "Vizuri sana. Asante," hakukuwa na maendeleo zaidi yaliyoripotiwa kwenye suala hilo. Netanyahu alikuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kumtembelea Trump baada ya tangazo la ushuru huo mpya, na ziara yake ilifuatiliwa kwa karibu duniani kote. Inaripotiwa pia kuwa alisafiri kwa njia ndefu zaidi kwa takriban kilomita 400 ili kuepuka uwezekano wa kukamatwa kutokana na hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Mbali na suala la ushuru, Trump alitoa kauli zilizoonekana kama 'mabomu' mbele ya Netanyahu. Mojawapo ilikuwa ni kuhusu Marekani kufanya "mazungumzo ya moja kwa moja na Iran." Kauli hii ilimfanya Netanyahu kuonekana kukosa raha na kubadilika sura yake mara moja. Chombo cha habari cha Israel, Ynet, kiliripoti kuwa Waziri Mkuu "alimeza mate, akaangalia kushoto na kulia, kisha akapanua macho, akakunja uso na kuinamisha kichwa." Baadaye, Netanyahu alijibu kwa tahadhari, "Ikiwa inaweza kufanywa kidiplomasia, ni jambo jema. Lakini lolote litakalotokea, ni lazima tuhakikishe Iran haipati silaha za nyuklia," akidokeza uwezekano wa hatua za kijeshi. Vyombo vya habari Israel vilionyesha wasiwasi kuwa mazungumzo ya Marekani na Iran yanaweza kudhoofisha uwezo wa Israel kuchukua hatua za kijeshi na kuhatarisha usalama wake.
Aidha, Trump alimsifu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, ambaye ni hasimu mkubwa wa Israel, akimuita "mwerevu sana." Trump alimwambia Netanyahu kuwa anaweza kuwa mpatanishi kati ya Israel na Uturuki, akisema, "Tatizo lolote linalohusiana na Uturuki, ikiwa utakuwa na busara, tunaweza kulitatua." Uturuki imekuwa ikiikoshoa vikali Israel, hasa kuhusu vita vya Gaza ambapo iliita Israel 'taifa la kigaidi', na uhasama wao umeongezeka tangu vita vya Syria.
Viongozi hao wawili walithibitisha misimamo yao iliyokubaliwa awali kuhusu suala la mateka wa Gaza na mipango ya ujenzi mpya. Awali, ilipangwa kufanyika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao, lakini ulifutwa takriban saa moja kabla.
Vyombo vya habari nchini Israel vilitoa tathmini kali na hasi kuhusu ziara hiyo. Gazeti la Times of Israel lilisema Netanyahu "atarejea nyumbani baada ya ziara ya kukatisha tamaa Marekani." Ynet iliripoti kuwa "(Netanyahu) alipata majibu ya kudhalilisha" na "hakupata chochote kihalisi." Gazeti la Hayom, katika makala yenye kichwa 'Kukumbatiwa kwa uchangamfu, ahadi zisizo wazi,' lilihoji, "Je, haya ndiyo matokeo aliyoyatarajia Netanyahu?" Gazeti la Haaretz lilienda mbali zaidi na kusema, "Rais Trump amepata fursa ya kuonyesha kwa muda kuwa mkakati wake wa kibiashara uliofeli umepata mafanikio, shukrani kwa mpinzani aliye tayari kunyoosha mkono kwake."