Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kuwa Iran ilitekeleza hukumu za kifo zisizopungua 975 mwaka jana, ikiweka rekodi ya "kiwango cha kutisha cha utekelezaji" wa hukumu hizo. Ripoti hiyo iliyotolewa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana António Guterres, pia imefichua uhalifu mwingine dhidi ya haki za kibinadamu, kuanzia kukandamiza uhuru wa kujieleza hadi mateso na kukamatwa na kufungwa kiholela.
Ripoti hii iliwasilishwa kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva mnamo Juni 18, 2025, na Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Nada Al-Nashif. Ripoti hiyo inaitaka serikali ya Iran kusitisha mara moja utekelezaji wote wa hukumu za kifo kama hatua ya kwanza kuelekea kuzipiga marufuku kabisa. Zaidi ya hayo, ripoti hiyo pia imetoa wito wa mazungumzo ya kidiplomasia ili kumaliza mashambulizi na mapigano yanayoendelea kati ya Iran na Israel.
Kulingana na ripoti ya Katibu Mkuu Guterres, idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka jana, yaani 975, inazidi kwa mbali rekodi ya mwaka 2023, ambapo watu 834 walinyongwa, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2015. Kati ya hukumu zilizotekelezwa mwaka jana, nne zilifanyika hadharani, na kwa kawaida hukumu za kifo nchini Iran hutekelezwa kwa kunyongwa.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa asilimia 52 ya watu walionyongwa walikuwa wamepatikana na hatia ya makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, asilimia 43 walikuwa wauaji, asilimia 2 walihusishwa na makosa ya unyanyasaji wa kingono, na asilimia 3 walihusika na masuala ya usalama.
Idadi ya wanawake walionyongwa pia imeongezeka. Kulingana na taarifa zilizopokelewa na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, wanawake wasiopungua 31 walinyongwa mwaka 2024, ikilinganishwa na 22 mwaka 2023. Kati ya wanawake hao 31, 19 walikuwa wamepatikana na hatia ya mauaji, huku 9 kati yao wakihukumiwa kifo kwa makosa ya kuwaua waume zao, mara nyingi kutokana na unyanyasaji wa nyumbani, ndoa za kulazimishwa, au ndoa za utotoni.
Miongoni mwa wale walionyongwa, kulikuwa na waandamanaji, wa kiume na wa kike, waliokamatwa wakati wa maandamano ya kupinga mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu, Mahsa Amini, ambaye alikamatwa na kuuawa na polisi wa maadili mnamo Septemba 2022 kwa kosa la kutovaa hijabu yake vizuri. Ripoti pia inaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu walionyongwa mwaka jana walitoka katika makabila madogodogo nchini Iran, huku wafungwa 108 wakiwa kutoka kabila la Baluchi na 84 wakiwa Wakurdi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, angalau wafungwa 31 wa kifo walikuwa wafungwa wa kisiasa na walinyongwa kuhusiana na masuala ya usalama wa taifa, ikiwemo tuhuma za ujasusi kwa niaba ya Israel. Ofisi hiyo pia imepokea ripoti za kesi ambazo hazikupata haki kutokana na mateso, kukamatwa bila hati ya mahakama, na hukumu zilizotolewa bila kufuata taratibu za kisheria.
Kuhusu uhuru wa kujieleza, haki ya kukusanyika, na maandamano ya amani, angalau waandishi wa habari 125 walishtakiwa mwaka 2024, na wanawake waandishi wa habari wasiopungua 40 walikamatwa na kuadhibiwa kuhusiana na kazi zao za uandishi.
Ingawa ripoti ya Al-Nashif imebainisha kuwa Iran imekuwa ikishirikiana kiasi fulani katika masuala ya haki za kibinadamu, Katibu Mkuu Guterres ameelezea masikitiko yake makubwa kwa serikali ya Iran kukataa kuwaruhusu wataalamu huru wa uchunguzi wa haki za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kuingia nchini humo. Hali hii inaendelea kuibua maswali mengi kuhusu hali halisi ya haki za kibinadamu nchini Iran.