Brice Oligui Nguema, kiongozi wa mpito wa taifa la Gabon lililopo Afrika ya Kati-Magharibi, amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo. Matokeo rasmi yaliyotangazwa yanaonyesha kuwa Nguema alijizolea asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa Jumamosi, Aprili 12, 2025.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mpinzani wake wa karibu, Alain-Claude Bilie By Nze wa upinzani, aliambulia asilimia 3 tu ya kura, akishika nafasi ya pili kwa mbali sana. Ushindi huu unampa Nguema uhalali wa kuongoza nchi hiyo baada ya kushika madaraka kama rais wa mpito kwa takriban miaka miwili.
Nguema aliingia madarakani mwezi Agosti 2023 kufuatia mapinduzi ya kijeshi. Mapinduzi hayo yalitokea baada ya rais wa wakati huo, Ali Bongo Ondimba, kutangazwa mshindi kwa muhula wa tatu katika uchaguzi uliozua utata mkubwa na madai ya udanganyifu. Jeshi, likiongozwa na Nguema ambaye wakati huo alikuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wa Jamhuri (Republican Guard), lilidai uchaguzi haukuwa huru na wa haki na likachukua madaraka.
Kitendo hicho cha mapinduzi kilihitimisha utawala wa familia ya Bongo uliodumu kwa miongo kadhaa nchini Gabon, tangu mwaka 1967 hadi 2023, kupitia marais wawili wa familia hiyo. Baada ya kuchukua madaraka, Nguema aliahidi kurejesha utawala wa kiraia kupitia uchaguzi.
Kabla ya uchaguzi huu, mnamo Novemba 2024, serikali ya mpito ilifanya mabadiliko kwenye katiba ya nchi. Mabadiliko hayo yalirefusha muda wa urais kutoka miaka mitano hadi miaka saba, na kuruhusu rais kuchaguliwa kwa mihula miwili. Baada ya mabadiliko hayo, ndipo uchaguzi huu uliitishwa na kufanyika.
Ushindi huu wa kishindo unampa Jenerali Nguema uhalali wa kisiasa ambao hakuwa nao alipokuwa akiongoza serikali ya mpito, na sasa anaanza rasmi muhula wake kama rais aliyechaguliwa na wananchi wa Gabon.
Chanzo cha picha: AFP