Hali ya kisiasa nchini Madagascar imeingia katika giza nene baada ya Rais Andry Rajoelina kutangaza rasmi kuwepo kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi linaloendelea nchini humo. Ofisi ya rais ilitoa taarifa kali ikilaani kile ilichokiita "jaribio la unyakuzi wa madaraka kinyume cha sheria na kwa kutumia nguvu," na kutoa wito kwa vikosi vyote vya kitaifa kuungana ili kulinda katiba na mamlaka ya nchi.
Ingawa taarifa hiyo haikumtaja moja kwa moja anayeongoza jaribio hilo la mapinduzi, ishara zote zinaelekea kwa kitengo maalum cha jeshi kinachojulikana kama CAPSAT. Wanajeshi hawa wasomi, ambao hapo awali walikuwa waaminifu kwa Rajoelina, wamegeuka na kuungana na maelfu ya vijana wanaoandamana barabarani wakimtaka rais ajiuzulu. Hii ni pigo kubwa kwa Rajoelina, kwani ni kitengo hichohicho kilichomsaidia kuingia madarakani mwaka 2009 kupitia mapinduzi.
Kwa takriban wiki tatu sasa, Madagascar imekumbwa na wimbi la maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Maandamano haya yanaongozwa na kundi la vijana lijulikanalo kama 'Gen Z Madagascar', ambao wamechoshwa na hali duni ya maisha, ukosefu wa ajira, na utawala wa Rajoelina. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 22 wamepoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa katika makabiliano na vyombo vya usalama, ingawa serikali bado haijathibitisha idadi hiyo.
Historia ya Rajoelina yenyewe imejaa misukosuko ya kisiasa. Aliingia madarakani kama kiongozi wa serikali ya mpito kufuatia mapinduzi ya mwaka 2009. Baadaye alishinda uchaguzi wa urais mwaka 2018 na akachaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2023. Hata hivyo, sasa anaonekana kuonja chungu ya dawa aliyowahi kuwanywesha wengine, huku jeshi lililombeba likionekana kuwa tayari kumtupa nje ya madaraka.