Ulimwengu wa walanguzi wakubwa wa madawa ya kulevya umepata pigo kubwa baada ya mmoja wa wahalifu waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba, raia wa China anayetambulika kama Zhang Zhi Dong, kukamatwa na hatimaye kusafirishwa kwenda nchini Marekani. Kukamatwa huku kumekuja kufuatia mchezo wa paka na panya uliovuka mipaka kadhaa baada ya mhalifu huyo kutoroka kizuizini nchini Meksiko.
Taarifa za kukabidhiwa kwake kwa Marekani zimethibitishwa na Waziri wa Usalama wa Meksiko, Omar Garcia Harfuch. Kupitia ujumbe kwenye mtandao wake wa X (uliojulikana zamani kama Twitter), Waziri Harfuch alifafanua kuwa mhalifu huyo wa kimataifa alinaswa na mamlaka nchini Cuba. Hii ilikuwa ni baada ya Zhang, aliyekuwa amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani (house arrest) katika jiji la Mexico City, kufanikiwa kutoroka na kutokomea kusikojulikana kabla ya kunaswa tena nchini Cuba mnamo Julai 31.
Ukubwa wa uhalifu wa Zhang, ambaye pia alifahamika kwa jina la utani 'Brother Wang', ni wa kiwango cha kutisha. Mamlaka nchini Meksiko zimeeleza kuwa yeye alikuwa mhusika mkuu katika usafirishaji na usambazaji wa shehena kubwa za madawa haramu. Anadaiwa kusimamia uingizaji wa Fentanyl kilo 1,800, Kokeni (Cocaine) kilo 1,000, na Methamphetamine (pia maarufu kama Philopon) zaidi ya kilo 600, kwenda Marekani na maeneo mengine.
Umuhimu wake katika mtandao huu haramu haukuwa wa kawaida. Serikali ya Marekani, hasa wakati wa utawala wa Donald Trump, ilimtaja Zhang kama kiungo muhimu zaidi kati ya wazalishaji wa kemikali ghafi za kutengeneza madawa nchini China na makundi ya kihalifu nchini Meksiko yanayotengeneza na kusambaza Fentanyl. Alifanya kazi kama dalali mkuu wa vifaa (logistics) na alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na makundi mawili hatari zaidi ya uhalifu nchini humo: Sinaloa Cartel na Jalisco New Generation Cartel (CJNG), ambayo yanajihusisha pia na mauaji ya kukodi (sicarrio).
Gazeti la Wall Street Journal (WSJ) linaripoti kuwa Idara ya Haki ya Marekani inamchukululia 'Brother Wang' kama mhalifu wa daraja la juu kabisa duniani, sawa na viongozi wakuu wa makundi hayo ya kihalifu ya Meksiko. Inadaiwa pia kuwa aliwahi kuwaleta "wakemia" (wataalamu wa kutengeneza madawa) kutoka China ili kutoa mafunzo kwa waendeshaji wa "maabara" (viwanda vya madawa) vya makundi hayo ya kihalifu.
Inakadiriwa kuwa kupitia mtandao wake huu wa kimataifa, waendesha mashtaka wa Meksiko wanaamini Zhang alikuwa akipata faida haramu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 150 (sawa na takriban Shilingi Bilioni 390 za Kitanzania) kila mwaka.
Zhang alihamia Meksiko kutoka China kabla ya janga la UVIKO-19. Ili kufanikisha shughuli zake na kujichanganya, alimuoa mwanamke wa Kimeksiko na kupata uraia wa nchi hiyo. Licha ya kuwa chini ya ulinzi akisubiri kusafirishwa kwenda Marekani, alifanikiwa kutoroka mwezi Julai. Mbio zake za kutoroka zilikuwa kama sinema; inaripotiwa alitumia ndege ya binafsi (private jet) kwenda Cuba, kisha akajaribu kwenda Urusi akitumia kitambulisho bandia. Aliponyimwa kuingia Urusi, alilazimishwa kurejea Havana, Cuba, ambapo ndipo alikamatwa.
Balozi wa Marekani nchini Meksiko, Ronald Johnson, alipongeza ushirikiano huo akisema "imefanyika kazi nzuri sana," na kuongeza kuwa "nchi zinaposhirikiana, wananchi ndio wanaonufaika."