Katika kile kinachoweza kutajwa kama "kuvunjika kwa mwiko" katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii, mtandao wa X (zamani Twitter) umefichua siri nzito iliyowaaibisha maelfu ya watumiaji waliokuwa wakijifanya wanaharakati wa siasa za Marekani. Imebainika kuwa wale "Wamarekani" wakali mnaoona wakibishana kwa Kiingereza 'cha kuunga' kuhusu Donald Trump au Joe Biden, kumbe wengi wao ni vijana waliokaa vijiweni Nairobi (Kenya), Lagos (Nigeria), na Mumbai (India) wakisaka 'mkwanja' wa mtandaoni.
Teknolojia Mpya Yaanika Uongo
Mtandao wa BBC umeripoti kuwa siri hii imefichuka baada ya mtandao wa X, unaomilikiwa na tajiri namba moja duniani Elon Musk, kuanzisha mfumo mpya wa 'uwazi' (transparency feature). Mfumo huu unaonyesha nchi halisi anayoishi mmiliki wa akaunti kwa kutumia taarifa za mtandao (IP address na VPN), hata kama kwenye wasifu (Bio) ameandika anaishi New York au Washington DC.
Hali hii imezua kicheko na mshangao. Kwa mfano, akaunti moja iliyojipatia umaarufu mkubwa kwa kujiita "Proud Democrat" (Mwanademokrasia Anayejivunia) na "MAGA Hunter" (Mwindaji wa wafuasi wa Trump), ilikuwa ikichochea mjadala mkali dhidi ya Trump. Watu waliamini ni mpiga kura wa Marekani, lakini mfumo mpya umemuumbua "mwamba" huyo na kuonyesha kuwa yuko nchini Kenya, akipiga kazi ya kibodi huku akifaidi upepo wa Afrika Mashariki.
"Trump Army" Kumbe Iko India
Vituko havikuishia hapo. Akaunti nyingine iliyokuwa na nguvu kubwa iitwayo "Trump_Army" (Jeshi la Trump), ilikuwa na wafuasi (followers) zaidi ya 500,000. Akaunti hii ilikuwa ikipost habari za kushangilia maamuzi ya Mahakama ya Juu ya Marekani na sera za Trump, kiasi kwamba hata vigogo wa Chama cha Republican walikuwa wakiifuatilia wakidhani ni 'Kamanda' wao wa Marekani.
Lahaula! Data za X zimeonyesha kuwa akaunti hiyo inaendeshwa kutokea nchini India. Baada ya kubumburuka kwa mchezo huo, mmiliki wa akaunti hiyo alilazimika kubadilisha haraka wasifu wake na kuandika: "Mhindi anayeipenda Marekani, Rais Trump, na Musk!"
Vilevile, akaunti maarufu ya "Ivanka News", iliyojifanya kuwa shabiki namba moja wa mtoto wa Trump, Ivanka, ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni moja, imebainika kuwa inaendeshwa kutokea nchini Nigeria. Akaunti hii ilikuwa ikihamasisha Wamarekani kupiga kura, kumbe "admin" yuko Lagos kwenye foleni za magari. X imechukua hatua ya kuifunga akaunti hiyo kwa muda usiojulikana.
Kwanini Wanafanya Hivi? Ni Dili la Pesa!
Swali la msingi ambalo wengi wanajiuliza ni, "Kwanini kijana wa Kenya au Nigeria ajifanye Mmarekani?" Jibu ni rahisi: Mpunga.
Tangu Elon Musk aanzishe utaratibu wa kugawa gawio la matangazo (Revenue Sharing) kwa watumiaji wanaopata 'engagement' (maoni, like, na share) kubwa, vijana wengi wamegeuza siasa za Marekani kuwa shamba la bibi. Wanajua kuwa Wamarekani ni wepesi wa kukasirika na kuchangia mada za kisiasa. Hivyo, vijana hawa wanatengeneza akaunti feki, wanaandika lugha za kuudhi au kusifia kupitiliza ili kupata 'views' nyingi, ambazo mwisho wa mwezi zinageuka kuwa Dola.
Huu ni mchezo wa "janja janja" ambao Watanzania tunauita "mjini shule." Wanatumia hisia za Wamarekani kutengeneza pesa za kuanzishia biashara huku Afrika na Asia.
Angalizo
Wataalamu wa usalama wa mtandao (Digital Forensics) wameonya kuwa, ingawa wengi wanafanya hivi kwa ajili ya pesa, kuna hatari ya vikundi vya kisiasa kutumia mwanya huu kupotosha maoni ya wapiga kura. BBC inaripoti kuwa kuna akaunti nyingine iliyojifanya ya "Mskochi" (Raia wa Scotland) ikipigania uhuru wa nchi hiyo, kumbe inaendeshwa kutokea Iran.
Tukio hili ni funzo kubwa: Usiamini kila unachokiona mtandaoni. Yule unayedhani ni mzungu anayekupa ushauri wa maisha, inawezekana ni jirani yako hapa hapa Tandale anayetafuta 'kiki' ya mtandaoni.