Taharuki na simanzi vimetawala nchini India baada ya mkutano wa kisiasa katika jimbo la Tamil Nadu kugeuka kuwa maafa, kufuatia msongamano mkubwa wa watu uliosababisha vifo vya takriban watu 39 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa vibaya.
Mkuu wa Jimbo la Tamil Nadu, M.K. Stalin, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo akitoa mchanganuo kuwa wahanga ni pamoja na wanaume 13, wanawake 17, wavulana wanne na wasichana watano. Aidha, ameeleza kuwa watu wengine 51, wakiwemo wanaume 26 na wanawake 25, wamelazwa na wanapatiwa matibabu ya kina katika vitengo vya wagonjwa mahututi.
Tukio hili la kusikitisha lilitokea katika eneo la Karur wakati wa mkutano wa kampeni wa Joseph Vijay, mwigizaji maarufu wa filamu aliyegeukia siasa na anayetarajiwa kuwania kiti katika uchaguzi wa jimbo hilo mwaka ujao. Vyombo vya habari vya nchini humo vinaripoti kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na umati wa watu unaokadiriwa kuzidi 30,000.
Video za tukio hilo zinaonyesha maelfu ya watu wakiwa wamezingira gari la kampeni la Vijay. Hali ilianza kuwa mbaya pale baadhi ya watu walipoanza kuzirai kutokana na msongamano na hewa nzito. Inasemekana kuwa Vijay, aliyekuwa juu ya gari, alianza kuwarushia chupa za maji, lakini punde si punde umati huo ulishindwa kudhibitika, na kumlazimu kuomba msaada wa haraka kutoka kwa polisi.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Vijay alielezea masikitiko yake makubwa akisema, "Moyo wangu umepasuka, nimezama kwenye maumivu yasiyovumilika na huzuni isiyoelezeka." Alituma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kuwaombea majeruhi wapone haraka.
Kufuatia mkasa huo, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, pia alitumia mtandao wa X kuelezea masikitiko yake, akiliita tukio hilo kuwa la "bahati mbaya sana."
Waziri Mkuu Stalin ameahidi kuunda tume maalumu ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha maafa haya na hatua zaidi zitachukuliwa baada ya ripoti kukamilika. Pia, alitangaza kuwa serikali itatoa fidia ya Rupia milioni moja (takriban Shilingi za Kitanzania milioni 31) kwa kila familia iliyopoteza mpendwa wao.
Hii si mara ya kwanza kwa mikutano ya Vijay kukumbwa na changamoto za kiusalama. Mnamo Oktoba mwaka jana, wakati akizindua chama chake kipya cha 'Tamilaga Vettri Kazhagam', watu wasiopungua sita walifariki dunia katika mkutano wake wa kwanza kutokana na miundombinu ya eneo husika kushindwa kuhimili umati mkubwa uliojitokeza.