Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umesitisha mpango wa kuhamisha wahamiaji haramu kwa kutumia ndege za kijeshi, hatua ambayo ililenga kuimarisha sera kali za uhamiaji. Kwa mujibu wa ripoti ya *Wall Street Journal (WSJ)*, Wizara ya Ulinzi ya Marekani haijatekeleza safari yoyote ya aina hiyo tangu Machi 1, huku ratiba ya ndege iliyopangwa Machi 6 pia ikifutwa.
Trump, tangu aingie madarakani Januari 20, ameendeleza msimamo mkali dhidi ya wahamiaji haramu. Mojawapo ya mikakati yake ilikuwa kutumia kituo cha Guantánamo Bay kama kituo cha mpito kwa wahamiaji waliokuwa wakisubiri kurejeshwa makwao. Kwa mfano, zaidi ya wahamiaji 200 wa Venezuela walihamishiwa Guantánamo kabla ya kusafirishwa hadi nchini mwao. Katika mchakato huu, serikali ya Marekani ilitumia ndege za kijeshi aina ya C-17 na C-130 Hercules kuwasafirisha wahamiaji hawa kuelekea Guantánamo au moja kwa moja katika mataifa yao ya asili.
Maafisa wa wizara ya ulinzi walieleza kuwa matumizi ya ndege za kijeshi yalikuwa pia na lengo la kuonyesha kwa uwazi msimamo mkali wa utawala wa Trump dhidi ya wahamiaji haramu. Uchunguzi wa *WSJ* ukitumia data za ufuatiliaji wa safari za ndege, ulibaini kuwa kulikuwa na takriban safari 30 za C-17 na safari 12 za C-130, huku nchi zilizohusika zikiwa ni pamoja na India, Guatemala, Ecuador, Peru, Honduras na Panama.
Hata hivyo, matumizi ya ndege hizi za kijeshi yameonekana kuwa ghali mno ikilinganishwa na njia za kawaida za kuwasafirisha wahamiaji. Kwa mfano, safari moja ya ndege ya kijeshi kwenda India iligharimu takriban dola milioni 3 (karibu Shilingi bilioni 4.3), huku gharama ya kusafirisha wahamiaji 12 kwenda Guantánamo ikiwa dola 20,000 kwa kila mtu (takriban Shilingi milioni 29). Ripoti ya *Reuters* iliongeza kuwa gharama ya kuendesha ndege ya C-17 ni dola 28,500 kwa saa (karibu Shilingi milioni 4.1), na kwamba gharama ya kusafirisha mhamiaji mmoja kwa ndege za kijeshi ilizidi hata bei ya tiketi ya daraja la kwanza kwenye ndege za abiria za kawaida.
Kutokana na gharama hizi kubwa, serikali ya Marekani imeamua kusitisha mpango huu, ingawa haijabainika iwapo utawala wa Trump utatafuta njia mbadala za kuendeleza sera yake kali ya uhamiaji.