Serikali ya Rais Donald Trump inaendelea kukiuka maamuzi ya mahakama kwa kushikilia msimamo wake wa kuwafukuza wahamiaji kwa wingi, jambo linalozidi kuzua mgogoro kati ya mhimili wa utawala na mahakama nchini Marekani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Wizara ya Sheria ya Marekani imekataa ombi la Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Washington D.C., James Boasberg, aliyekuwa akihitaji taarifa za safari ya ndege iliyowasafirisha wahamiaji wa Venezuela waliotimuliwa kuelekea El Salvador. Jaji Boasberg alitaka kujua muda wa kuondoka na idadi ya wahamiaji waliokuwemo kwenye ndege hiyo, lakini serikali ilikataa kutoa taarifa hizo, ikisema kuwa ni "kuingilia mamlaka ya utawala wa rais kwa njia isiyokubalika."
Serikali ya Trump imesisitiza kuwa uamuzi wa mahakama unaingilia mamlaka yake katika masuala ya usalama wa taifa, diplomasia, na sera za kigeni. Wizara ya Sheria iliwasilisha nyaraka mahakamani ikidai kuwa, "Mahakama haina mamlaka ya juu zaidi kuliko serikali, na kuendelea kwake kuingilia maamuzi ya utawala ni jambo lisilokubalika."
Katika uamuzi wa awali, Jaji Boasberg alikuwa ameagiza serikali isimamishe mpango wa kuwahamisha raia wa Venezuela kwa madai kwamba walikuwa sehemu ya genge la uhalifu la "Tren de Agua." Pia, aliamuru kuwa iwapo ndege ya kuwarejesha El Salvador ilikuwa tayari imeondoka, basi irudishwe Marekani. Hata hivyo, serikali ya Trump ilikaidi agizo hilo na kuendelea na mpango wa kuwahamisha wahamiaji hao.
Mnamo Machi 18, Rais Trump alimshambulia Jaji Boasberg, akisema kuwa anapaswa kuondolewa madarakani kwa sababu ya uamuzi wake huo. Hata hivyo, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu, John Roberts, alitoa tamko la nadra, akipinga wito wa Trump wa kutaka Boasberg aondolewe, akisema kuwa madai hayo "hayafai na hayana msingi."
Msemaji wa White House, Caroline Leavitt, alipoulizwa kuhusu hatma ya safari za kuhamisha wahamiaji wakati kesi inaendelea mahakamani, alisema: "Kwa sasa hakuna ndege maalum iliyoratibiwa, lakini mpango wa kuwaondoa wahamiaji utaendelea."
Leavitt aliendeleza mashambulizi dhidi ya mahakama, akidai kuwa majaji wanaompinga Trump wanafanya kazi kwa niaba ya chama cha Democratic. Alisema kuwa "asilimia 60 ya maagizo ya mahakama yaliyolenga kumzuia Trump yametolewa katika kipindi cha karne hii, na asilimia 92 ya maagizo hayo yametolewa na majaji walioteuliwa na Democrats."
Alimshutumu Jaji Boasberg kwa kuwa na mwelekeo wa kisiasa na kudai kuwa "amekuwa akipinga sera za Trump kwa muda mrefu." Pia, alidai kuwa mke wa jaji huyo aliwahi kuchangia zaidi ya dola 10,000 kwa chama cha Democratic, jambo alilosema linaonyesha upendeleo wa kisiasa.
Leavitt alisisitiza kuwa serikali itaheshimu maagizo ya mahakama lakini pia itaendelea kupambana kisheria. "Tutaendelea kupinga uamuzi huu mahakamani na ikiwa itahitajika, tutakwenda hadi Mahakama ya Juu kuhakikisha tunashinda."
Mvutano kati ya utawala wa Trump na mahakama unaendelea kuzidi kupamba moto, huku pande zote zikiwa na misimamo mikali kuhusu hatima ya wahamiaji wanaoishi nchini Marekani bila vibali.