Rais wa Marekani, Donald Trump, amezua gumzo la kimataifa baada ya kumsifu Rais wa Liberia, Joseph Boakai, kwa ustadi wake wa kuongea lugha ya Kiingereza, akionekana kutofahamu kuwa Kiingereza ndiyo lugha rasmi ya taifa hilo la Afrika Magharibi. Tukio hili la kushangaza lilitokea Ikulu ya White House wakati wa chakula cha mchana na viongozi kadhaa wa Afrika.
Katika hafla hiyo, baada ya Rais Boakai kumaliza kutoa hotuba yake fupi, Rais Trump alionekana kuvutiwa sana. Tofauti na viongozi wengine wawili waliomtangulia ambao walihitaji wakalimani, Boakai alizungumza kwa Kiingereza fasaha. "Asante. Hicho ni Kiingereza kizuri sana," Trump alisema.
Kisha, kwa mshangao, Trump alianza kumhoji Rais Boakai. "Ulijifunza wapi Kiingereza hicho kizuri? Ni wapi?" aliuliza. Baada ya kimya kidogo, Trump aliuliza tena kwa msisitizo, "Ulipata elimu? Wapi?" Rais Boakai alijibu kwa upole, "Ndio, Mheshimiwa Rais." Trump akauliza tena, "Nchini Liberia?" na Boakai akathibitisha tena, "Ndio, Mheshimiwa Rais."
Huku akionyesha kustaajabu, Trump alimalizia kwa kusema, "Inavutia sana. Kiingereza ni lugha nzuri, kuna watu kwenye meza hii hawakizungumzi vizuri kama wewe." Wakati wote wa maswali hayo, Rais Boakai alitabasamu kwa heshima bila kumweleza Rais Trump kwamba Kiingereza ndiyo lugha rasmi nchini Liberia tangu taifa hilo lilipoasisiwa.
Historia inaonyesha kuwa Liberia ilianzishwa mwaka 1822 na watu weusi waliokuwa watumwa nchini Marekani, ambao walihamia Afrika na kuanzisha nchi yao. Walitangaza uhuru mwaka 1847 na wamekuwa wakitumia Kiingereza kama lugha rasmi tangu wakati huo.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Trump kutoa maoni yanayoonekana kuwakosoa watu wengine kuhusu matumizi yao ya Kiingereza. Katika mkutano na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alimlalamikia mwandishi wa habari kutoka India akisema, "Sikuelewi kabisa. Lafudhi yako inafanya iwe vigumu kukuelewa." Katika tukio jingine, alimtaka mwandishi mwingine wa Kihindi atafutiwe mkalimani ingawa alikuwa akiuliza swali kwa Kiingereza.
Wasifu wa Rais Boakai unaonyesha kuwa ni kiongozi msomi aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika sekta binafsi. Inajulikana kuwa alisafiri kwa miguu umbali wa zaidi ya kilomita 500 kutoka kijijini kwake hadi mji mkuu, Monrovia, kutafuta elimu.