Kimenuka rasmi kati ya kampuni ya OpenAI (watengenezaji wa ChatGPT) na mahakama ya Marekani. Kampuni hiyo imegoma katakata kutii amri ya jaji inayowataka kuwasilisha kumbukumbu za mazungumzo (logs) ya watumiaji wake milioni 20 kwa kampuni ya habari ya New York Times (NYT). OpenAI wamesema amri hii ni hatari na inafungua mlango wa kukiuka faragha za mamilioni ya watu duniani kote.
Katika nyaraka walizowasilisha mahakamani huko New York, mawakili wa OpenAI wameomba amri hiyo ifutwe mara moja. Wanadai kuwa kuwalazimisha kukabidhi mazungumzo ya faragha ya watu kwa mhusika mwingine (NYT) ni "mfano mbaya na hatari." Walisisitiza kuwa kesi ya msingi ya hakimiliki inayowakabili na NYT inahusu asilimia ndogo sana (chini ya 0.01%) ya mazungumzo hayo. "Mengi ya mazungumzo haya hayana uhusiano wowote na kesi hii; ni mazungumzo ya kibinafsi na ya siri ya watu," walisema. OpenAI waliongeza kuwa hali hii inawaweka watumiaji wote walioongea na ChatGPT katika miaka mitatu iliyopita kwenye hatari ya mazungumzo yao kuchunguzwa bila sababu za msingi, wakiiita "hitaji la kupita kiasi na lisilo la haki."
Chanzo cha mzozo huu ni kesi ya msingi ambayo NYT waliifungua dhidi ya OpenAI, wakiwashutumu kwa kutumia maelfu ya makala zao bila ruhusa kufundisha ChatGPT. NYT waliomba mahakama iamuru OpenAI kuhifadhi mazungumzo hayo ili yasifutwe, wakidai ni ushahidi muhimu katika kesi yao. Jaji Ona Wang wa Mahakama ya Wilaya ya Kusini mwa New York alikubaliana na ombi hilo. Jaji Wang aliamuru OpenAI kukabidhi kumbukumbu hizo, lakini kwa sharti moja: ziwe zimefichwa utambulisho (anonymized) ili majina ya watumiaji na taarifa zao binafsi zisionekane. Jaji aliona kuwa hatua hiyo inatosha kulinda faragha za watumiaji.
Suala hili sasa limehama kutoka chumba cha mahakama na kuwa la umma. Mkuu wa Usalama wa Taarifa wa OpenAI, Dane Stuckey, aliandika kwenye blogu ya kampuni hiyo akisisitiza: "Tutapambana vikali dhidi ya jaribio hili la NYT la kukiuka faragha ya watumiaji wetu."
Hata hivyo, NYT wamejibu mapigo vikali. Msemaji wa kampuni hiyo alisema OpenAI "wanawapotosha watumiaji." Walifafanua kuwa mahakama imeagiza sampuli ndogo tu, iliyofichwa utambulisho kikamilifu na OpenAI wenyewe, na data zote zitalindwa na amri maalum ya mahakama. "Hakuna faragha ya mtumiaji itakayokiukwa. OpenAI wanajaribu kukwepa kiini cha kesi," alisema msemaji huyo. Mahakama imewapa OpenAI hadi leo, Novemba 14, kutekeleza amri hiyo, na sasa macho yote yanaelekezwa kwao kuona kama watatii au wataendeleza msimamo wao.