Tanzania imepata heshima ya kipekee katika medani ya kimataifa baada ya Chuo chake cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) kuchaguliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mwenyeji wa mafunzo adimu kwa maafisa wanadhimu wa jeshi kutoka mataifa mbalimbali duniani. Mafunzo haya yanalenga kuwatayarisha maafisa hao kuwa wakufunzi wa kimataifa.
Akizindua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Brigedia Jenerali George Itang’are, alieleza kuwa hii ni mara ya pili tu kwa mafunzo haya kufanyika duniani kote tangu Umoja wa Mataifa upitishe mtaala mpya wa mafunzo ya kijeshi. Alisema Tanzania inakuwa nchi ya pili, baada ya Italia, kupata heshima ya kuandaa mafunzo haya ya ngazi ya juu.
"Hii ni ishara ya imani kubwa ambayo Umoja wa Mataifa unayo kwa jeshi letu na kwa taifa letu kwa ujumla. Tunajivunia kuwa sehemu ya kuwajengea uwezo maafisa hawa wenye uzoefu ili wakafundishe wengine katika nchi zao," alisema Brigedia Jenerali Itang'are.
Kozi hiyo ya siku 10, inayofanyika kuanzia Julai 7 hadi 17 na kufadhiliwa na Serikali ya Canada, inawakutanisha maafisa wanadhimu 22 kutoka nchi za Ghana, Nigeria, Botswana, Vietnam, Zambia na mwenyeji Tanzania. Wakufunzi wa kozi hiyo wanatoka nchi za Tanzania, Brazil, Bangladesh, Nigeria na Marekani, kuonyesha sura halisi ya ushirikiano wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma Jumuishi za Mafunzo kutoka Umoja wa Mataifa, Harinder Sood, alisema Tanzania ilichaguliwa kutokana na historia yake ndefu na ya kuigwa katika kushiriki operesheni za ulinzi wa amani duniani, pamoja na kuwa nchi yenye utulivu na mazingira rafiki.
“Misheni za ulinzi wa amani za sasa zina changamoto nyingi, hivyo tunahitaji maafisa waliobobea. Mafunzo haya yatazalisha wakufunzi watakaosaidia kuandaa vikosi vyenye weledi wa hali ya juu, na Tanzania ni mshirika muhimu katika kufanikisha hili," alisema Sood.
Kuaminiwa kwa JWTZ kuendesha mafunzo haya kunathibitisha weledi wa jeshi la Tanzania na mchango wake unaoendelea katika kuhakikisha amani na usalama duniani.