Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Simon Pigapiga, amewahimiza maofisa wa Jeshi waliomaliza mafunzo ya soka la ufukweni kuanzisha timu za mchezo huo ndani ya vikosi mbalimbali vya Jeshi, ili kuchochea ushindani na maendeleo ya mchezo huo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Utawala na Rasilimali Watu Jeshini, Meja Jenerali Michael Gaguti, Brigedia Jenerali Pigapiga alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya siku 10 yaliyowahusisha wahitimu 24 wa mchezo wa soka la ufukweni.
Alieleza kuwa soka la ufukweni linatoa fursa kwa vijana, sio tu katika kukuza vipaji vyao, bali pia kama chanzo cha ajira na njia ya kukuza utalii wa ndani kupitia mashindano ya kitaifa na kimataifa.
"Endeleeni kueneza mafunzo haya kwa askari wenzetu. Mlifundishwa kuwa makocha, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha mnawafundisha wengine na kuanzisha timu katika vikosi vyenu. Tunataka kuona matokeo chanya ya mafunzo haya," alisema Brigedia Jenerali Pigapiga.
Aliongeza kuwa timu hizo hazipaswi kuanzishwa tu katika maeneo yenye bahari, bali pia katika maeneo yenye maziwa, ili kuhakikisha mchezo huo unasambaa na kukua kote nchini.
Zaidi ya hayo, alifichua kuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, ametoa pongezi za dhati kwa wahitimu wote waliomaliza kozi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Brigedia Jenerali Pigapiga alisisitiza kuwa soka la ufukweni linahitaji sio tu ujuzi wa kawaida, bali pia nidhamu ya mwili, mbinu maalum, na uelewa wa kipekee wa mazingira ya uwanja wa mchanga. Aliahidi kuwa JWTZ itaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadau wengine mbalimbali ili kuhakikisha mchezo huo unapata msukumo na maendeleo makubwa zaidi.
Jeshi, kwa kushirikiana na TFF, limeanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya mchezo huo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja maalum, kama kile cha Mbweni Ndege Beach ambacho kiko katika hatua nzuri za kukamilika.
Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema kuwa baada ya kufanya utafiti wa kina, waligundua kuwa mataifa mengine yanaendeleza mchezo huo kwa kutumia askari wa Jeshi, hivyo wakaona umuhimu wa kushirikiana na JWTZ.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo ni hatua ya awali, na kwamba kuna mipango ya kuleta mkufunzi wa kimataifa, Twalib Bilal, ambaye ni Mtanzania lakini pia mkufunzi wa soka la ufukweni kwa Bara la Asia, ili kuwanoa zaidi wanajeshi hao.
Mafunzo haya yameratibiwa na TFF kwa kushirikiana na JWTZ kwa lengo la kutimiza azma ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, ya kuhakikisha Jeshi linakuwa mstari wa mbele katika kushiriki michezo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.