Kila ifikapo tarehe 7 Septemba, jumuiya ya kimataifa huungana kutambua umuhimu wa ushirikiano baina ya majeshi ya polisi duniani, katika Siku ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Polisi. Siku hii, iliyoasisiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2022, inatoa fursa ya kutafakari jukumu la Polisi wa Kimataifa (Interpol) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1923, na kusisitiza umuhimu wa mshikamano katika vita dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka.
Ingawa Tanzania bado haijaanza kuadhimisha siku hii kwa kiwango cha kitaifa, Jeshi la Polisi nchini ni mnufaika mkubwa na mshiriki hai wa mtandao huu wa usalama duniani. Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime, anathibitisha kuwa ushirikiano huu umekuwa na tija kubwa, ukichangia kulifanya jeshi kuwa la kisasa, lenye maafisa weledi na linaloweza kukabiliana na changamoto za kiusalama za karne ya 21.
Kupitia ushirikiano huu, Tanzania ni mwanachama hai wa jumuiya muhimu za kipolisi za kikanda kama vile Shirikisho la Wakuu wa Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki (EAPCCO) na lile la Kusini mwa Afrika (SARPCCO). Uanachama huu umewezesha maafisa wa Tanzania kupata mafunzo maalum ya kukabiliana na uhalifu wa kupangwa kama biashara haramu ya dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu, na uhalifu wa kimtandao.
Zaidi ya hapo, uanachama wa Tanzania katika Interpol tangu mwaka 1967 umezaa matunda yanayoonekana. Jeshi la Polisi limepata teknolojia za kisasa, ikiwemo mfumo wa mawasiliano salama wa I-24/7. Mfumo huu unaunganisha Tanzania na nchi karibu 197 duniani, ukirahisisha ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia kwa haraka kuhusu wahalifu wanaotafutwa au mali za wizi kama magari. Hii ina maana kwamba, hata raia anayetaka kununua gari kutoka nje anaweza kupata uhakika wa usalama wa chombo hicho kupitia jeshi la polisi.
Mafanikio haya hayapo kwenye makaratasi pekee. Operesheni za pamoja zimefanikiwa kuvunja mitandao ya wahalifu, kama ile ya mwaka 2024 iliyohusisha Tanzania, Kenya na Uganda na kufanikisha kukamatwa kwa mamia ya kilo za dawa za kulevya. Vilevile, Tanzania imejipambanua kwa mchango wake katika ulinzi wa amani duniani, ambapo maafisa wake, hususan wanawake, wameshiriki katika misheni za Umoja wa Mataifa na kupata sifa kwa kazi yao.
Licha ya hatua hizi kubwa za mafanikio, bado kuna safari ndefu katika kuimarisha uwajibikaji na haki za binadamu ndani ya jeshi hilo. Ripoti mbalimbali zinaendelea kuibua maswali kuhusu matumizi ya nguvu na ukosefu wa chombo huru cha kuchunguza malalamiko dhidi ya polisi. Hii ni changamoto ambayo inahitaji kufanyiwa kazi ili kuendana na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyesisitiza kuwa polisi wanapaswa kujenga uaminifu na mshikamano na jamii wanayoihudumia.