Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepata pigo baada ya askari wake wawili kupoteza maisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walipokuwa wakitekeleza jukumu la ulinzi wa amani.
Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, aliwasilisha salamu za rambirambi pamoja na ubani kwa familia za askari hao waliopoteza maisha kutokana na mapigano kati ya kikundi chao na waasi wa M23.
Askari hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Tanzania kilichopo DRC kwa mujibu wa makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kusaidia kurejesha utulivu katika taifa hilo jirani linalokumbwa na machafuko ya mara kwa mara. Tanzania, ikiwa miongoni mwa mataifa yenye msimamo wa kusaidia kulinda amani barani Afrika, pia inashiriki katika operesheni za ulinzi wa amani nchini Lebanon, Afrika ya Kati, Msumbiji na maeneo mengine yenye changamoto za kiusalama.
Tunapongeza ujasiri wa JWTZ na mchango wake mkubwa katika juhudi za kuimarisha amani si tu katika ukanda wa Afrika Mashariki, bali pia katika bara lote. Kitendo cha Tanzania na mataifa mengine kujitoa kulinda amani katika nchi zenye migogoro kinaonyesha mshikamano wa kweli wa Kiafrika na kuthibitisha msemo kuwa "Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja."
Tunazitakia faraja familia za mashujaa hawa waliopoteza maisha na kuwatia moyo wanajeshi waliobaki kuendelea na jukumu lao la kulinda amani bila kukata tamaa.
Hata hivyo, ni muhimu kwa mataifa yanayokumbwa na migogoro kutafakari athari za vita na umwagaji damu. Historia inaonyesha kuwa mara nyingi mapigano haya hunufaisha mataifa au makundi yanayotaka kuuza silaha au kunyonya rasilimali za nchi hizo.
Tunazihimiza serikali za Afrika, EAC, SADC na Umoja wa Afrika kwa ujumla kuongeza juhudi za kidiplomasia ili kupata suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa DRC. Hatua hizi zisiishie kwenye juhudi za kijeshi pekee, bali pia zijikite katika mazungumzo na usuluhishi wa kweli.
Tunawahakikishia JWTZ na mataifa yote yanayoshiriki katika kulinda amani kuwa juhudi zao zinathaminiwa na Afrika nzima. Tunawaombea kwa Mungu awape nguvu, busara na ulinzi katika kazi yao njema ya kutetea amani barani.