Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imetoa tamko kali kulaani tabia ya baadhi ya vijana kutoka Kenya wanaotumia mitandao ya kijamii kumdhalilisha na kumvunjia heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Dk. Alhad Mussa Salum, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza kuwa jumuiya hiyo imeshtushwa na lugha ya kashfa na matusi inayotolewa dhidi ya Rais Samia, ambayo imehusishwa na vijana wa nchi jirani ya Kenya.
"Sisi kama JMAT tunaamini kwamba Kenya ina viongozi wa dini na serikali wenye ushawishi. Tunawaomba sana wazungumze na vijana wao na kuwasihi waache tabia hii ya kumvunjia heshima Rais wa nchi nyingine, ikiwemo Rais wa Tanzania," alisema Sheikh Salum. Alionya kuwa tabia ya matusi na dharau dhidi ya viongozi wa mataifa mengine si tu inakiuka misingi ya heshima na uhusiano mzuri wa kidiplomasia, bali pia ni kosa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Sheikh Salum alisisitiza kuwa heshima ya taifa lolote inategemea maadili ya raia wake. "Tuwakumbushe kwamba heshima ya taifa lolote ni maadili ya watu wake. Ikiwa Wakenya wataendelea na matusi dhidi ya viongozi wa mataifa mengine, basi si tu watakuwa wanamkosea Mungu kwa kuwatusi wazazi wao, bali pia watakuwa wanapoteza ustaarabu wao mbele ya uso wa dunia," aliongeza.
Alionya kuwa hali hii isipuuzwe, kwani inaweza kusababisha mtafaruku wa kijamii na kidiplomasia ikiwa haitadhibitiwa mara moja. "Tulipofika panatosha. Moto mkubwa huanza kama cheche ndogo, hivyo ipo haja ya kuzizima cheche hizi kabla hazijakuwa moto mkubwa," alihitimisha.
JMAT imetoa wito kwa wananchi wote wa Afrika Mashariki kutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya heshima, uadilifu na maadili, ili kulinda misingi ya amani na mshikamano katika ukanda huo. Jumuiya hiyo inaamini kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa chombo muhimu cha kuimarisha uhusiano kati ya nchi na watu, lakini matumizi mabaya yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Hali hii inakuja wakati ambapo uhusiano kati ya Tanzania na Kenya umeimarika katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na biashara na ushirikiano wa kiuchumi. Vitendo vya vijana wachache havipaswi kuruhusiwa kuharibu uhusiano huu mzuri. JMAT inasisitiza umuhimu wa mazungumzo na diplomasia katika kutatua masuala yanayohusu uhusiano kati ya nchi.