Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, amethibitisha kuhudhuria kama mgeni rasmi katika Mashindano ya Dunia ya Kusoma Qur’an Tukufu, yatakayofanyika Februari 23, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Tukio hili linatarajiwa kuwa la kihistoria, likiwaleta pamoja washiriki kutoka mabara yote matano duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi, alieleza kuwa mashindano haya ni ya kipekee kutokana na ushiriki mpana wa mabara yote. "Hii ni mara ya kwanza kuona mashindano ya aina hii yakivutia washiriki kutoka Afrika, Asia, Ulaya, nchi za Kiarabu, na Amerika. Hii inadhihirisha juhudi za Rais Samia katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kuhamasisha umoja na undugu kati ya mataifa," alisema Mufti Zuberi.
Mufti Zuberi alitumia fursa hiyo kuwasihi wazazi kuwekeza katika elimu ya dini kwa watoto wao. "Tunawahimiza wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema kwa kuwaelekeza kwenye elimu ya dini. Hii itasaidia kujenga taifa lenye maadili na linalomcha Mungu," alisisitiza.
Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Balozi wa Saudi Arabia, Sheikh Mutab Bin Azamay Suleiman, alitoa pongezi kwa Tanzania kwa kuendelea kuwa nchi ya amani na utulivu. "Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa amani na utulivu, na ndiyo maana imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano haya makubwa ya kimataifa," alisema Sheikh Suleiman. Aliongeza kuwa Waziri Mkuu wa Saudi Arabia amesaini mikataba ya ushirikiano kati ya BAKWATA na serikali ya Saudi Arabia, na mashindano haya ni moja ya matunda ya ushirikiano huo.
Sheikh Othuman Kaporo, ambaye ni mratibu wa mashindano hayo, alifahamisha kuwa tukio hilo litahudhuriwa na Imam Mkuu wa Msikiti wa Madina, Sheikh Abdallah Buaijan. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupata ugeni wa aina hiyo.
Washindi wa mashindano hayo watapata zawadi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na magari, bajaji, pikipiki, na tiketi za kwenda kuhiji Makka. Zaidi ya hayo, kutakuwa na huduma za kupima afya bure kwa magonjwa yasiyoambukiza kwa wale watakaohudhuria mashindano hayo.
Mashindano haya yanatarajiwa kuwa tukio kubwa la kidini na kimataifa, linalolenga kuhamasisha usomaji wa Qur’an na kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu duniani.