Hali ya hofu, simanzi na taharuki imegubika taifa la Nigeria, ambalo mara nyingi hujulikana kama 'Jitu la Afrika', kufuatia taarifa mpya za kushtua zinazohusu tukio la kinyama la utekaji nyara katika Shule ya Bweni ya St. Mary's. Wakati dunia ikiwa bado inatafakari idadi ya awali iliyotajwa, Chama cha Kikristo nchini humo (CAN) kimefanya uhakiki wa kina na kubainisha kuwa hali ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa; idadi kamili ya roho zilizoshikiliwa na watekaji imefikia watu 315.
Tukio hili la kusikitisha lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Jimbo la Niger, ambapo makundi ya watu wenye silaha yalivamia shule hiyo ya Kanisa Katoliki na kuondoka na nusu ya idadi ya wanafunzi wote shuleni hapo. Awali, iliripotiwa kuwa watu takriban 227 ndio walikuwa wametekwa, lakini baada ya CAN kupitia daftari la mahudhurio na kufanya mawasiliano na wazazi, ukweli mchungu umebainika.
Kwa mujibu wa takwimu hizo mpya zilizotolewa na CAN na kuripotiwa na shirika la habari la AFP, waliotekwa ni wanafunzi 303 (mchanganyiko wa wavulana na wasichana) pamoja na walimu 12, ambapo kati yao wanawake ni wanne na wanaume wanane. Hii ina maana kuwa karibu nusu ya wanafunzi 629 wa shule hiyo hawajulikani walipo, jambo ambalo limeacha vidonda visivyopona kwa wazazi na walezi.
'Ugonjwa' wa Utekaji Wasambaa Tukio hili la St. Mary's si la kubahatisha, bali linaonekana kuwa sehemu ya wimbi jipya la uhalifu uliokithiri. Wiki hii pekee imekuwa ya damu na machozi nchini humo. Mnamo Novemba 17, wanafunzi wa kike 25 walitekwa katika shule moja ya sekondari jimboni Kebbi, Kaskazini-Magharibi mwa nchi hiyo. Siku moja baadae, Novemba 18, ibada katika kanisa moja Magharibi mwa Nigeria iliingia doa baada ya wanamgambo kuvamia, kuua waumini wawili na kuteka makumi ya wengine.
Kutokana na hali hii ya hatari, sekta ya elimu nchini Nigeria imeingia 'shakani'. Mamlaka katika majimbo ya Katsina na Plateau zimetangaza kufunga shule zote kama hatua ya dharura ya kunusuru maisha ya watoto. Shirika la habari la Bloomberg limebainisha kuwa shule 47 za bweni zinazomilikiwa na Serikali ya Shirikisho zimeomba kufungwa kwa muda, zikihofia usalama wa wanafunzi. Hii ni pigo kubwa kwa "kizazi cha kesho" cha taifa hilo.
Rais Tinubu Aweka Mpira Kwapani Kutokana na uzito wa janga hili, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, amelazimika kufanya maamuzi magumu. Rais Tinubu amefuta safari yake muhimu ya kuelekea nchini Afrika Kusini, ambako alitazamiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi (G20) unaofanyika Novemba 22 na 23, 2025.
Uamuzi huu wa Tinubu unaonyesha kuwa nyumba inapoawaka moto, huwezi kwenda kusaidia kuzima moto wa jirani. Badala ya kwenda Johannesburg kujadili uchumi wa dunia, Rais huyo sasa amejikita katika vikao vya dharura vya baraza la usalama la taifa ili kutafuta mbinu za kijeshi na kiintelijensia za kuwakomboa mateka hao na kurejesha amani iliyotoweka.
Trump Aingilia Kati Katika hatua nyingine inayoongeza joto la kimataifa, Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa kauli nzito akilaani vitendo hivyo. Trump, ambaye utawala wake umekuwa ukisisitiza uhuru wa kuabudu, ameonya kuwa Marekani haitasita kuchukua hatua za kijeshi ikiwa vitendo vya mauaji na utekaji dhidi ya Wakristo vitandelea kufumbiwa macho na makundi ya kigaidi yenye mlengo wa kiislamu nchini humo. Kauli hii ya Trump inaongeza shinikizo kwa serikali ya Tinubu kuhakikisha inamaliza tatizo hili haraka kabla halijageuka kuwa mgogoro wa kimataifa.
Wakati dunia ikiwa imelekeza macho yake Afrika Kusini kwa ajili ya G20, Nigeria inabaki ikilia, huku wazazi 315 wakiwa hawana usingizi, wakisubiri kwa hamu kuona watoto na wapendwa wao wanarejea salama.