Kufuatia kukamatwa kwa zaidi ya tani 30 za dawa mpya ya kulevya aina ya 'Kratom' nchini, Tanzania imechukua hatua madhubuti katika medani ya kimataifa kwa kuingia makubaliano na nchi ambako mmea huo unazalishwa ili kudhibiti biashara yake haramu. Hatua hii ni matokeo ya ushiriki wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwenye Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC39) uliofanyika nchini Marekani.
Akizungumza baada ya mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA), Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema ushirikiano huo mpya utasaidia kuziba mianya ya dawa hiyo hatari ya ‘Mitragyna Speciosa’ kuingia nchini, ambayo hata katika nchi inakotoka imeorodheshwa kama dawa hatari.
Mbali na ishu ya Kratom, ujumbe wa Tanzania ulifanikiwa pia kuingia makubaliano muhimu na nchi zinazozalisha kwa wingi kemikali bashirifu—malighafi zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya kama heroini na kokeini. Lengo ni kudhibiti mtiririko wa kemikali hizo na kuvuruga mtandao wa utengenezaji wa 'unga' duniani.
Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa mkutano huo umefungua milango mipya ya ushirikiano, akisifu jitihada za kidiplomasia za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo zimewezesha Tanzania kupata mafanikio hayo. Alisema dunia sasa inakabiliwa na changamoto mpya, ikiwemo biashara ya dawa za kulevya kuhamia kwenye majukwaa ya kidijitali na mbinu mpya za kisayansi za kutengeneza dawa hizo.
"Tumejifunza umuhimu wa kuwekeza katika upelelezi wa kisayansi kupitia ‘forensic intelligence’ na matumizi ya vifaa vya kisasa kubaini dawa hizi mipakani. Mbinu za kizamani pekee hazitoshi tena," alisema Kamishna Lyimo.
Miongoni mwa mafanikio ya haraka yaliyopatikana ni pamoja na makubaliano na shirika la kimataifa la INL, ambalo limeahidi kusaidia kuimarisha Maabara ya Taifa ya Vipimo vya Jinai. Vilevile, DCEA imekubaliana na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Nigeria (NDLEA) kuharakisha mkataba wa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, ambazo zote zinakabiliwa na tatizo la usafirishaji wa dawa za kulevya.