Ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, katika jiji la Mumbai, India, ambapo alishiriki Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Masuala ya Habari, Filamu na Burudani (World Audiovisual & Entertainment Summit – WAVES), imefungua milango mingi ya fursa kwa Tanzania, hasa katika kuendeleza sekta za habari, filamu, sanaa na burudani.
Profesa Kabudi alibainisha fursa hizi muhimu Mei 3, 2025, mara baada ya kumaliza mazungumzo ya kando na Waziri wa Nchi, Wizara ya Habari na Utangazaji wa India, Dkt. Roganathan Murugan. Katika kikao hicho chenye tija, mawaziri hao wawili walikubaliana hatua kadhaa za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao katika nyanja hizo za ubunifu na mawasiliano.
Makubaliano makuu ni pamoja na kufufua upya Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la India, All India Radio (AIR). Hatua hii itafanywa kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa lengo la kuwezesha Lugha ya Kiswahili kutangazwa tena na Radio hiyo yenye ushawishi mkubwa nchini India na kusikika katika Bara Hindi na maeneo mengine duniani kote ambako matangazo ya All India Radio hufika. Hii ni fursa kubwa ya kutangaza na kukuza Lugha ya Kiswahili kimataifa.
Aidha, mawaziri hao waliafikiana kuanzisha ushirikiano wa kiufundi, hasa katika teknolojia za kisasa za utangazaji wa redio ya kidijitali. Profesa Kabudi alieleza kuvutiwa kwake na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na India katika mfumo wa utangazaji wa kidijitali wa DRM 30+. Alieleza kuwa ujumbe wake ulipata fursa ya kutembelea maonesho na kujionea jinsi India ilivyo mbele sana kiteknolojia katika kurusha matangazo ya redio, akisisitiza kuwa ushirikiano huu utaiwezesha Tanzania kujifunza na kuboresha miundombinu yake ya utangazaji.
Maeneo mengine muhimu ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni katika sekta ya filamu. Tanzania na India zimekubaliana kuchunguza njia za kushirikiana katika utengenezaji wa filamu, kubadilishana maudhui, na kusaidiana katika usambazaji wa filamu. Hii inajumuisha jitihada za kuhakikisha filamu za Kitanzania zinafika na kuuzika katika soko kubwa la India, huku filamu za Kihindi zikiendelea kununuliwa na kutumiwa nchini Tanzania kama ilivyozoeleka.
Ili kuwezesha filamu za Kitanzania kupenya zaidi katika soko la India, Profesa Kabudi alitaja mkakati wa kuongeza maneno ya tafsiri (subtitles) kwa lugha za Kihindi na Gujirati kwenye filamu zinazotengenezwa Tanzania. Hatua hii ni muhimu sana kuondoa kikwazo cha lugha na kufanya filamu hizo zieleweke na kuuzika kwa urahisi nchini India. Vilevile, walijadili uwezekano wa taasisi mpya ya India inayojihusisha na sanaa bunifu na teknolojia kuchukua wanafunzi kutoka Tanzania kwa ajili ya mafunzo. Chuo hiki kipya kinasisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa, ambazo Profesa Kabudi aliziona kuwa muhimu sana kwa wasanii wa Tanzania kujifunza na kuzitumia kuboresha kazi zao za sanaa na kufanya tafiti za kina katika fani zao.
Katika jitihada za kukuza utalii na sekta ya filamu nchini, Profesa Kabudi alitumia fursa hiyo kumkaribisha Waziri wa India na watengenezaji wa filamu kutoka nchini humo kutumia maeneo ya kimkakati na yenye mandhari ya kuvutia nchini Tanzania kwa ajili ya kurekodi filamu zao, hususan zile za Kihindi. Alitaja maeneo mashuhuri kama Mlima Kilimanjaro, eneo la hifadhi la Ngorongoro, Zanzibar, na maeneo mengine mazuri kama vivutio vinavyofaa kwa shughuli za utengenezaji filamu. Pia aliwaalika watu mashuhuri wa India, wakiwemo waigizaji na watayarishaji wa filamu, kuja kutembelea Tanzania ili wajionee maeneo hayo na kuona uwezekano wa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.
Katika kuimarisha zaidi kubadilishana kwa kitamaduni na kibiashara, Tanzania imevialika taasisi za filamu za India kushiriki katika maonesho makubwa ya filamu yanayofanyika Tanzania kila mwaka, kama vile Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) na Sinema Zetu. Kwa upande wao, India pia imetoa mwaliko kwa Tanzania kushiriki katika maonesho yao ya filamu, ambayo mara nyingi hufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba.
Mbali na kushiriki Mkutano Mkuu wa WAVES na kufanya mazungumzo ya kando na Waziri wa India, Profesa Kabudi na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea maonesho mbalimbali yaliyoandamana na mkutano huo. Pia walitembelea eneo maarufu la Bollywood, ambalo ndilo kitovu cha tasnia ya filamu nchini India. Ziara hii ilikuwa na lengo la kujifunza mengi, hasa yanayohusu ujenzi wa studio na miundombinu, ambayo yatasaidia wakati Tanzania inajenga Kituo chake cha Sanaa na Michezo (Arts and Sports Arena). Ushirikiano huu unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa na kuinua viwango vya sekta za habari, filamu na burudani nchini Tanzania.