Katika hotuba kali na ya kipekee, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, ametoa uchambuzi wa kina kuhusu dhana ya "Taifa," akisema Tanzania inasimama yenyewe kama Taifa halisi barani Afrika, huku nchi nyingine nyingi zikiwa ni "mikusanyiko ya makabila."
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Julai 9, 2025, mbele ya wadau wa habari waliojadili Uchaguzi Mkuu ujao, Profesa Kabudi alihoji kuwa upekee wa Tanzania unatokana na misingi yake imara ambayo haipaswi kulegalegeshwa. Alisema nguvu ya Tanzania inajengwa juu ya nguzo kuu mbili: Muungano wa hiari na nguvu ya lugha ya Kiswahili. Alifafanua kuwa Taifa la Tanzania ni matokeo ya ridhaa ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, na si mpango wa kulazimishwa.
Nguzo ya pili, aliyoielezea kwa kina, ni lugha ya Kiswahili. "Kiingereza kimewafanya wengine kuwa mkusanyiko wa makabila, lakini Kiswahili kimetufanya sisi kuwa Taifa moja," alisema Profesa Kabudi. Aliongeza kuwa hata kama wapo wanaoidharau Tanzania kwa kutokimudu Kiingereza, ukweli ni kwamba Kiswahili ndicho kimekuwa gundi imara iliyounganisha makabila zaidi ya 160 na tamaduni zake tofauti kuwa kitu kimoja chenye mwelekeo wa pamoja. Alionya kuwa, "Tusipoelewa hili, tutaanza kuiga na kuwaabudu wenye mikusanyiko ya makabila."
Akiendelea kufafanua, Profesa Kabudi alisisitiza kuwa kila Taifa linalojitambua lina alama na tunu zake ambazo lazima ziliindwe kwa wivu mkubwa. Akitolea mfano Mwenge wa Uhuru, Profesa Kabudi alikwenda mbali zaidi akisema, kuna vitu ambavyo kwa wengine vinaweza kuonekana kama "upuuzi" au hata "ujinga," lakini kwa Taifa lenye kujitambua, ndiyo nguzo muhimu zinazobeba heshima na utambulisho wake.
"Moja ya jambo linaloweza kuonekana ni ujinga ni Mwenge wa Uhuru, lakini ni muhimu sana kwa Tanzania. Kila taifa lazima liwe na 'ujinga' wake unaoheshimiwa, ambao kwa hakika ndio unaolifanya liendelee kuwa Taifa," alisisitiza. Alimalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania, hasa wanahabari, kuulinda umoja na utaifa huo, akionya kuwa kuanza kudharau alama za taifa ni mwanzo wa kubomoa misingi ya nchi.