Katika kile kinachoweza kutajwa kama "kufunga breki ya ghafla" kwenye mbio za teknolojia ya magari duniani, kampuni nguli ya utengenezaji magari kutoka Marekani, Ford Motor Company, imetangaza mabadiliko makubwa ya kimkakati ambayo yameacha midomo wazi wadau wa sekta ya magari. Ford wameamua kupunguza kasi ya uwekezaji kwenye magari ya umeme (EV) na badala yake kuelekeza nguvu kwenye magari ya mseto (Hybrid) na yale ya mafuta, uamuzi uliogharimu kampuni hiyo hasara ya kutisha ya Dola za Marekani bilioni 19.5, sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 52.6.
Hatua hii ya Ford inatafsiriwa na wachambuzi wa uchumi kama ishara tosha kuwa soko la magari ya umeme bado ni "kigugumizi" na halijatengamaa kama ilivyotarajiwa, hasa kutokana na kupungua kwa kasi ya mauzo na mabadiliko ya sera za kiserikali nchini Marekani.
F-150 Lightning: Kutoka 'Star' hadi Kusitishwa
Mhanga mkubwa wa mabadiliko haya ni lori la kifahari aina ya 'Ford F-150 Lightning'. Hili ni gari ambalo liliingia sokoni mwaka 2022 kwa mbwembwe nyingi, likisifiwa na mastaa wakubwa akiwemo mchekeshaji Jimmy Fallon ambaye hata alilitungia wimbo. Agizo la awali liligonga ‘oda’ laki mbili, na kuifanya Ford kuongeza uzalishaji haraka. Lakini, kama wahenga wasemavyo, "ngoma ikivuma sana hupasuka."
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mauzo ya gari hilo yameporomoka kwa asilimia 10 hadi kufikia Novemba mwaka huu, zikiwa zimeuzwa unit 25,583 pekee. Kutokana na hali hiyo, Ford wamesitisha uzalishaji wa F-150 la umeme tupu na sasa wanahamia kwenye teknolojia ya EREV (Extended Range Electric Vehicle). Hii ni teknolojia ambapo gari linatumia umeme, lakini lina injini ndogo ya mafuta (generator) kwa ajili ya kuchaji betri likiwa safarini—mfumo ambao unawavutia zaidi madereva wasio na uhakika wa vituo vya kuchaji.
Kufa kwa Mradi wa T3 na Kiwanda cha Tennessee
Maumivu hayajaishia hapo. Mradi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu wa lori la kizazi kipya la umeme, lililopewa jina la msimbo 'T3', umefutwa rasmi. Mradi huu ulitarajiwa kuwa mkombozi katika kiwanda chao kipya huko Tennessee. Badala yake, Ford wamebadili gia angani na kutangaza kuwa kuanzia mwaka 2029, kiwanda hicho kitazalisha malori mapya ya kutumia mafuta (petroli/dizeli). Hii ni habari njema kwa wapenzi wa 'ungurumo' za injini, lakini ni pigo kwa wanaharakati wa mazingira.
Aidha, Ford imesitisha pia mpango wa kutengeneza mabasi madogo ya biashara (Vans) ya umeme. Mkakati mpya ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, asilimia 50 ya magari yao yanakuwa ni mchanganyiko wa Hybrids, EREVs, na ya umeme kamili, badala ya kutegemea umeme pekee.
Mgawanyo wa Hasara ya Trilioni 52
Uamuzi huu mgumu haujaja bure. Hesabu za mezani zinaonyesha kuwa Ford itabeba mzigo wa hasara kama ifuatavyo:
- Trilioni 22.9 (Dola 8.5bn) zimetokana na kufutwa kwa miradi ya magari ya umeme iliyokuwa imeanza.
- Trilioni 16.2 (Dola 6bn) ni gharama za kuvunja ubia na kampuni ya kutengeneza betri ya SK On kutoka Korea Kusini.
- Trilioni 13.5 (Dola 5bn) ni gharama za programu nyinginezo zilizofutwa.
Siasa na Soko la Marekani
Mabadiliko haya pia yanachochewa na upepo wa kisiasa nchini Marekani. Tangazo la kuondolewa kwa ruzuku na punguzo la kodi kwa wanunuzi wa magari ya umeme kumesababisha mauzo kushuka kwa asilimia 40 mwezi Novemba pekee. Pia, kulegezwa kwa masharti ya utoaji wa hewa chafu (emissions) kumewapa watengenezaji "kichwa" cha kuendelea kutengeneza magari ya injini za kawaida ambayo bado yanapendwa na wengi kutokana na nguvu na uimara wake.
Kwa sasa, Ford imeweka wazi kuwa itaendelea kuajiri maelfu ya wafanyakazi wapya kwa ajili ya miradi hii mipya ya Hybrid na mafuta, huku ikipunguza baadhi ya wafanyakazi katika viwanda vya betri. Hii ni ishara kuwa, licha ya kelele za kutunza mazingira, biashara ya magari bado inatawaliwa na mahitaji halisi ya mteja na faida.