Katika hatua isiyotarajiwa inayoashiria mabadiliko ya kimkakati katika vita vya teknolojia kati ya Marekani na China, serikali ya Rais Donald Trump imeruhusu kampuni ya Nvidia kuanza tena kuuza chipu zake za Akili Mnemba (AI) aina ya 'H20' nchini China. Imefichuka kuwa uamuzi huu ni sehemu ya makubaliano mapana ya kibiashara ili kuishawishi China ianze tena kuiuzia Marekani madini adimu ya sumaku (rare earth magnets).
Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, alithibitisha waziwazi mpango huo. "Tulijumuisha suala hili katika mazungumzo ya kibiashara ya sumaku," aliliambia shirika la habari la Reuters, akifafanua kuwa ni "biashara ya kubadilishana" yaani, 'chipu kwa sumaku'.
Kampuni ya Nvidia, ambayo ni kinara duniani katika utengenezaji wa chipu za AI, ilikuwa imezuiwa na serikali ya Marekani kuuza chipu za H20 nchini China tangu mwezi Aprili, na hivyo kupoteza mapato ya mabilioni ya dola. Baada ya uamuzi huu mpya, thamani ya hisa za Nvidia ilipanda kwa asilimia 4.
Uamuzi huu ni wa kipekee kwa sababu serikali za Marekani, zote mbili za sasa na iliyopita, zimekuwa zikizuia vikali uuzaji wa teknolojia za hali ya juu, hasa chipu za AI, kwenda China kwa sababu za kiusalama wa taifa. Wachambuzi wanauona uamuzi huu kama ishara ya "nia njema" kutoka kwa Marekani katika mchakato mpana wa mazungumzo ya kibiashara na China.
Hata hivyo, hatua hii imezua ukosoaji mkubwa ndani ya Bunge la Marekani. Baadhi ya wabunge wameonya kuwa kuruhusu chipu hizi kuingia China ni "hatua potofu" inayompa mpinzani teknolojia ya hali ya juu. Wana wasiwasi kuwa ingawa chipu za H20 hazina nguvu sana katika 'kufunza' mifumo ya AI, zina uwezo mkubwa katika awamu ya 'utendaji' (inference) na zinaweza kutumika kujenga kompyuta zenye nguvu za ajabu (supercomputers).
Uamuzi huu umekuja wiki moja tu baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Nvidia, Jensen Huang, kukutana na Rais Trump na kumshawishi kuwa ili Marekani iendelee kuongoza soko la AI, ni lazima kampuni zake ziruhusiwe kuuza bidhaa zao kote duniani. Kwa sasa, Bwana Huang yuko Beijing kwa mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya China, akisisitiza umuhimu wa soko la China, ambalo linachangia asilimia 13 ya mapato yote ya Nvidia, sawa na dola bilioni 17 (takriban Shilingi trilioni 44.2 za Kitanzania).
Kufuatia habari hizi, kampuni hasimu ya Nvidia, AMD, nayo imetangaza kuwa imeomba kibali cha kuuza chipu zake za AI nchini China, na kusababisha hisa zake pia kupanda kwa asilimia 7.