Hatimaye kilio cha muda mrefu cha kampuni ya Nvidia kimesikika Ikulu ya Marekani. Katika uamuzi uliostua soko la teknolojia na siasa za kimataifa, Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuruhusu mauzo ya chipu (vifaa vya kompyuta) zenye nguvu kubwa aina ya 'H200' kwenda China, lakini kwa sharti zito la kulipa ushuru wa asilimia 25.
Hatua hii imefungua tena milango ya mabilioni ya dola kwa Nvidia, ambayo ilikuwa imepoteza soko la China kutokana na vikwazo vya awali, na inatafsiriwa kama ushindi mkubwa wa jitihada za ushawishi (lobbying) zilizofanywa na kampuni hiyo.
Trump: "Nimeongea na Rais Xi, Tumekubaliana"
Kupitia mtandao wake wa Truth Social siku ya Jumapili (Desemba 8), Trump alitangaza uamuzi huo akisema: "Ninaruhusu mauzo ya H200 kwenda China, lakini kutakuwa na ada ya asilimia 25."
Rais Trump aliongeza kuwa amemtaarifu Rais wa China, Xi Jinping, kuhusu uamuzi huo na kwamba kiongozi huyo wa China "ameupokea kwa mtazamo chanya." Trump alitetea kodi hiyo ya 25% akisema inalenga:
- Kulinda usalama wa taifa la Marekani.
- Kutengeneza ajira kwa Wamarekani.
- Kuhakikisha Marekani inaendelea kuwa kinara wa teknolojia ya AI huku ikipata faida ya kiuchumi.
Mchakato wa Kiuendeshaji: 'Mzigo' Lazima Upitie Marekani
Ili kudhibiti usalama, utaratibu mpya utakuwa hivi: Chipu hizo zikishatengenezwa na kiwanda cha TSMC (Taiwan), zitasafirishwa kwanza kwenda Marekani. Huko zitatozwa hiyo kodi ya 25% na kufanyiwa ukaguzi wa kiusalama, ndipo ziruhusiwe kusafirishwa kwenda China. Hii inahakikisha Marekani inaona kila kifaa kinachoenda Beijing.
Nvidia imepokea habari hizi kwa shangwe, ikiita "maelewano yenye tija." Soko la hisa nalo liliitikia haraka, ambapo hisa za Nvidia zilipanda kwa asilimia 3 mchana na kuongezeka tena usiku, ishara kuwa wawekezaji wamefurahia kurejea kwa soko la China.
Mtego wa "Vifaa vya Kati"
Wachambuzi wa mambo wanasema hii ni mbinu ya kijanja ya Marekani inayoitwa "Middle Ground Strategy."
- Kilichozuiwa: Marekani bado imepiga marufuku kabisa kuuza chipu mpya na zenye nguvu zaidi kuliko zote duniani, 'Blackwell', kwenda China.
- Kilichoruhusiwa: Wameruhusu toleo la nyuma yake kidogo (H200).
Lengo ni kuipa China teknolojia nzuri (H200 ina nguvu mara 6 zaidi ya H20 iliyokuwa ikitumika China), lakini kuwanyima ile teknolojia ya juu kabisa (Blackwell). Hii inalenga kuifanya China isihangaike kutengeneza chipu zake (kama inavyofanya Huawei), huku Marekani ikiendelea kuwa mbele kiteknolojia.
China: Kufa Kufaana?
China inakabiliwa na wakati mgumu. Makampuni yake yana kiu kubwa ya chipu za AI. Mtaalamu wa masuala ya usalama, Chris Maguire, anasema: "China kukataa ofa hii itakuwa ni kujiumiza yenyewe (self-harm)."
Hata hivyo, bado kuna wasiwasi wa kiusalama. China imekuwa ikihofia kuwa chipu za Marekani zinaweza kuwa na "milango ya siri" (backdoors) ya udukuzi. Serikali ya Beijing itapaswa kupima kati ya hitaji la kukuza uchumi wa AI na fahari ya kutaka kujitegemea.
Upinzani Ndani ya Marekani
Si wote wamefurahia. Wanasiasa wenye msimamo mkali kama Seneta Elizabeth Warren wameonya kuwa kuuzia China H200 ni kuwapa silaha adui. "Hii itaharakisha uwezo wa kijeshi wa China kwenye AI," alionya Warren.
Licha ya kelele hizo, Nvidia inaonekana kushinda vita hii ya kisiasa, kwani Bunge la Marekani hivi karibuni lilifuta mswada uliolenga kubana mauzo hayo (GAIN AI Act), ikionyesha nguvu ya ushawishi wa kampuni hiyo.
Kwa ufupi, Trump ameamua kufanya biashara na adui yake wa kiteknolojia: "Ukitaka teknolojia yetu, lipa kodi, na tutakupa ile ambayo sisi tumeshaanza kuiona ya zamani."