Bendera Yapaa Paris: Tanzania Yaukwaa Ujumbe Mzito UNESCO, Sasa Kuamua Hatima ya Urithi wa Dunia

international | Mon Nov 24 2025


Bendera Yapaa Paris: Tanzania Yaukwaa Ujumbe Mzito UNESCO, Sasa Kuamua Hatima ya Urithi wa Dunia

Katika kile kinachotajwa kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia na sifa kedekede kwa sekta ya utalii na mambo ya kale nchini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kushinda kiti nyeti cha Ujumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia (World Heritage Committee) chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).


Ushindi huo wa kishindo umepatikana katika uchaguzi mkali uliofanyika Novemba 24, 2025, jijini Paris nchini Ufaransa, ambapo wajumbe wa mataifa mbalimbali walipiga kura ya imani kwa Tanzania kuingia katika chombo hicho chenye maamuzi mazito kuhusu hazina za dunia. Hatua hii inaifanya Tanzania kuwa mmoja wa waamuzi wakuu wa masuala ya urithi wa kimataifa kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.


Jukumu Zito Mabegani mwa Tanzania Kuingia kwa Tanzania katika kamati hiyo si jambo dogo. Kamati ya Urithi wa Dunia ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuamua ni eneo gani duniani linastahili kupewa hadhi ya kuwa "Urithi wa Dunia". Hii ina maana kwamba, kwa miaka minne ijayo, Tanzania itakuwa na sauti katika kupitisha au kukataa maombi ya nchi wanachama wanaotaka maeneo yao yatambulike kimataifa.


Jukumu hili linakuja wakati muafaka ambapo Tanzania imekuwa ikijipambanua katika kuhifadhi rasilimali zake, ikiwa ni nyumbani kwa vivutio vinavyotambulika na UNESCO kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Mji Mkongwe wa Zanzibar, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, pamoja na Hifadhi ya Ngorongoro. Uwepo wa Tanzania katika meza ya maamuzi unatoa fursa ya kujifunza zaidi na kusimamia viwango vya uhifadhi kwa jicho la karibu.


Mlinzi wa 'Thamani ya Kipekee ya Ulimwengu' Miongoni mwa kazi kubwa ambazo wawakilishi wa Tanzania wataifanya ni pamoja na kuchakata mapendekezo mapya na kuamua yapi yanakidhi vigezo vya kile kinachoitwa kitaalamu "Outstanding Universal Value" (Thamani ya Kipekee ya Kibinadamu). Siyo kila eneo linaweza kuingia kwenye orodha hii; lazima liwe na sifa za kipekee ambazo kupotea kwake kutaacha pengo lisilozibika katika historia au jiografia ya dunia.


Aidha, nafasi hii inakuja na jukumu la 'upolisi'. Kamati hii ndiyo yenye wajibu wa kufuatilia hali ya uhifadhi wa maeneo yote ambayo tayari yamo kwenye orodha. Hii inamaanisha kuwa Tanzania itashiriki katika kutathmini ripoti za uharibifu au tishio lolote linalokabili maeneo ya urithi duniani, iwe ni kutokana na vita, mabadiliko ya tabianchi, au shughuli za kibinadamu, na kutoa maelekezo ya nini kifanyike kuokoa jahazi.


Fursa kwa Utalii na Diplomasia Wadadisi wa mambo ya kimataifa wanaona ushindi huu kama matunda ya Tanzania kujifungua zaidi duniani (Royal Tour effect) na kuimarisha diplomasia yake. Kushiriki katika vikao vya kamati hii kutaweka jina la Tanzania midomoni mwa jumuiya ya kimataifa mara kwa mara, jambo ambalo ni mtaji tosha wa kuitangaza nchi kiutalii bila gharama ya ziada.


Ni heshima ambayo inathibitisha kuwa dunia inatambua mchango wa Tanzania katika kutunza urithi wa asili na utamaduni, na sasa imepewa rungu la kusaidia mataifa mengine kufanya hivyo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.